NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akiweka udongo katika Kaburi la aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Amani Abdi Ali Mzee ‘Mrope’ aliyezikwa leo Kijijini kwao Jumbi Unguja.
VIJANA Maalum wa UVCCM wakiwa na Jeneza la Marehemu Abdi Ali Mzee kwa ajili ya Mazishi huko Jumbi Unguja.
……………………
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi, leo ameongoza Maelfu ya Wananchi katika Mazishi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Amani Unguja Marehemu Abdi Ali Mzee ‘Mrope’ aliyefariki jana akiwa katika Matibabu huko katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es saalam na amezikwa leo kijijini kwao Jumbi Mkoa wa Kusini Unguja.
Viongozi mbali mbali wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali wameshiriki mazishi hayo wakiwemo Katibu wa NEC,Idara ya Organazasheni Makao Makuu Ndugu Pereira Ame Silima,Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa CCM Zanzibar Mwl.Kombo Hassan Juma pamoja na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe.Zubeir Ali Maulid.
Wengine ni Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mawaziri na Manaibu Mawaziri, Wabunge na Wawakilishi,Wakurugenzi wa Idara mbali mbali za SMZ,Wenyeviti na Makatibu wa CCM wa ngazi mbali mbali, Wana CCM na Wananchi kwa ujumla.
Katibu wa UVCCM Wilaya ya Amani Ndugu Mohamed Ali Mohamed,akisoma wasifu wa marehemu amesema CCM na Jumuiya zake wamepokea kwa Huzuni na Masikitiko Taarifa ya Kifo cha Mwenyekiti huyo wa CCM Wilaya ya Amani Unguja.
Alisema Mwenyekiti Abdi Ali Mzee alizaliwa mwaka 1964 katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja na kupata Elimu yake ya Msingi kuanzia mwaka 1978 katika Skuli ya Msingi Kidongo Chekundu pamoja na kupata Elimu ya Sekondari katika Skuli ya Shangani mwaka 1981.
Pia alieleza kwamba Abdi mwaka 1984 alijiunga na Chuo cha Ufundi wa Chuma huko Chang’ombe Dar es saalam na kujiunga rasmi na Chama Cha Mapinduzi mwaka 1983 katika Tawi la CCM Sogea.
Katika maelezo yake Katibu huyo, ameeleza kuwa Marehemu Enzi za Uhai wake alishika nyadhifa mbali mbali katika Chama mwaka 1992 hadi 2007 alikuwa Balozi wa Nyumba 10 Shina namba 7 katika Tawi la CCM la Sogea,mwaka 1997 hadi 2007 alikuwa Mwenyekiti wa CCM Tawi la Sogea,mwaka 2007 hadi mwaka 2012 alikuwa ni Mwenyekiti wa Jimbo la Magombeni.
Alieleza kuwa mwaka 2012 hadi mwaka 2019 alikukuwa ndiye Mwenyekiti wa mwanzo toka kuanzishwa kwa Wilaya Mpya ya Amani na pia alikuwa Mkufunzi wa Makada katika Chuo cha Itikadi cha CCM,Mjumbe wa Bodi ya kudhibiti kodi za Nyumba Zanzibar.
Pamoja na hayo Mwenyekiti huyo licha ya kuwa Mwanasiasa pia alikuwa ni Mwanamichezo Mstaafu wa Mpira wa Miguu aliyewahi kuchezea Timu za African Kids,Wazee Sports Club hadi umauti unamkuta alikuwa ni Mwalimu wa Timu ya New Boko kutoka Mtaa wa Boko Zanzibar.
Sambamba na hayo Chama Cha Mapinduzi Taifa kupitia Mwenyekiti wake Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein wanatoa Salamu za Pole kwa Wafiwa Ndugu,Jamaa,Marafiki na Watu wote walioguswa na Msiba huo na kuwaomba waendelee kuwa na subra katika kipindi hiki cha Maombolezo.
Marehemu ameacha Vizuka wawili na Watoto Saba.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahala Pema Peponi Amin.