Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kuwait, Israel ,Brazil na Urusi walipokwenda kumuaga Ikulu Chamwino mkoani Dodoma. Januari 26,2022.Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza na Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kuwait, Israel ,Brazil na Urusi walipokwenda kumuaga. Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma. Januari 26,2022.
***********************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali,mazungumzo yaliofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma. Mabalozi hao ni wale wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kuwait, Israel ,Brazil na Urusi.
Makamu wa Rais amewapongeza Mabalozi hao kwa kuteuliwa na imani waliopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuliwakilisha taifa kwenye nchi hizo. Makamu wa Rais amewasihi Mabalozi kwenda kufanya kazi kwa weledi na uzalendo kwa maslahi ya taifa.
Amesema ni muhimu kwa Mabalozi hao kuendeleza na kukuza ushirikiano baina ya Tanzania na nchi wanazokwenda kuliwakilisha taifa.
Makamu wa Rais amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo mkubwa katika kutekeleza diplomasia ya uchumi hivyo amewataka Mabalozi hao kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi utakaokuwa na manufaa kwa Tanzania.
Aidha amewaasa Mabalozi hao kutambua vipaumbele vya taifa ikiwa ni pamoja na kufahamu takwimu za msingi ikiwemo Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020, Dira ya taifa na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano zitakazochagiza katika kutafuta wawekezaji.
Amesema ni muhimu kwa Mabalozi hao kufanya jitihada za makusudi kuzifahamu vema nchi wanazokwenda kuiwakilisha Tanzania ili kuweza kujifunza misingi ya ukuzaji wa uchumi wao na kuhamisha maarifa hayo kwa taifa la Tanzania. Amesema katika kutekeleza diplomasia ya uchumi Mabalozi hao wanapaswa kuongeza ushirikiano na vongozi wa sekta binafsi ili kuwavutia kuwekeza Tanzania.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imeweka msisitizo katika kuleta mabadilizo katika uwekezaji pamoja na kuimarisha sekta ya viwanda hivyo amewasihi mabalozi hao kujielekeza katika kutafuta teknolojia rafiki zitakazosaidia katika kukuza na kuendeleza viwanda kulingana na mazingira ya hapa nchini.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amewaagiza Mabalozi hao Kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini pamoja na kutafuta fursa za ushirikiano hasa katika taasisi za utafiti na maendeleo.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba Mabalozi wanapaswa kutafuta fursa mbalimbali kwa nchi ya Tanzania ikiwemo kuwavutia watalii. Amewasihi kuhakikisha wanashiriki katika mikutano mbalimbali itayowezesha kueleza mazuri ya Tanzania pamoja kuvutia wawekezaji. Amesema ni muhimu kuendelea kuitangaza lugha ya Kiswahili katika nchi hizo ikiwemo kutafuta fursa ya kufundishwa kwa lugha hiyo katika nchi wanazokwenda kuiwakilisha. Aidha amewaagiza kutafuta fursa za ajira na elimu kwa watanzania.
Aidha amesema Mabalozi wanapaswa kuwaunganisha watanzania wanaoishi katika nchi wanazokwenda kuwakilisha ili kuwa na mawazo ya pamoja namna wanavyoweza kuwekeza hapa nchini na kurudisha ujuzi na maarifa walioyonayo nyumbani Tanzania.
Makamu wa Rais amewasihi Mabalozi hao kuwa na nidhamu ya matumizi ya pesa zinazopelekwa katika kuendesha Balozi hizo ili kuongeza tija ya uwakilishi katika vituo vyao.
Akishukuru kwa niaba ya mabalozi hao Balozi wa Tanzania nchini Brazil Prof. Adelardus Kilangi amemshukuru Makamu wa Rais kwa maelekezo na kuahidi kwenda kufanya kazi kwa bidii, weledi na maarifa katika kuiwakilisha Tanzania katika nchi hizo.