Mratibu wa mfuko wa maendeleo ya jamii(Tasaf)mkoa wa Ruvuma Xsaveria Mlimira kulia,akizungumza na wanufaika wanaopokea fedha za ruzuku katika kijiji cha Chiwana Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani humo wakati wa zoezi la malipo kwa walengwa wa kijiji hicho.
Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Nchini(Tasaf)mkoani Ruvuma Xsaveria Mlimira kulia akimsikiliza mlengwa wa kaya maskini wa kijiji cha Chikomo kata ya Chiwana Halmashauri ya wilaya Tunduru Ali Wadali kuhusiana na changamoto mbalimbali inayowakabili walengwa wa mfuko huo ikiwamo kuchelewa kwa ruzuku na kukosekana kwa kadi za matibabu.
**************************
Na Muhidin Amri,
Tunduru
MRATIBU wa mfuko wa Maendeleo ya jamii nchini(Tasaf)mkoa wa Ruvuma Xsaveria Mlimira,amewaasa wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini wanaopokea ruzuku ya fedha kutoka Tasaf kuanzisha miradi ya kimkakati na biashara ndogo ndogo ili kuwaingizia kipato.
Mlimira ameyasema hayo kwa nyakati tofauti,wakati akizungumza na wanufaika wa mpango huo katika kijiji cha Chikomo na Chiwana kata ya Chiwana Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani humo.
Alisema, walengwa wakiwa na miradi ya kiuchumi kama ya ufugaji na mama lishe wataweza kumudu maisha yao ya kila siku bila shida, hata pale mpango wa kupokea fedha kutoka Serikalini utakapokoma(kumalizika).
Amewashauri kuanzisha vikundi vya kupeana na kukopeshana ambavyo vina umuhimu mkubwa kwenye familia na jamii hasa yenye kipato cha chini kupata fedha za kujikimu kimaisha na kufanya mambo mbalimbali ya maendeleo.
Aidha,amewakumbusha kujiwekea akiba na kutumia fedha hizo kwa malengo, badala ya kuzielekeza katika anasa ikiwamo ulevi na wanaume kuoa mke zaidi ya mmoja kwani tabia hiyo inachangia kuongeza umaskini katika jamii.
Alisema, malengo ya Serikali kutoa fedha kupitia Tasaf ni kuona kila kaya ina uwezo wa kupata milo mitatu kwa siku,wananchi wapate huduma za matibabu na watoto wanaosoma wapate mahitaji ya shule na mavazi.
Akizungumzia changamoto ya walengwa kukosa kadi za Bima ya afya licha ya kuchangishwa fedha Mlimira, amewatoa hofu na kueleza kuwa tatizo hilo litakwisha kwani liko ya chini ya uwezo wake na kuwataka kuendelea kuchangia ili waweze kupata matibabu.
Baadhi ya wanufaika wa Tasaf, wameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuona umuhimu wa kuendelea kutoa fedha ambazo zimesaidia kuboresha maisha yao.
Hadija Hamis alisema, kupitia fedha za Tasaf amefanikiwa kujenga nyumba ya matofari na kuezeka bati na kuanzisha biashara ya kufuga kuku ambao unamwezesha kupata fedha za kujikimu na familia yake na kuiomba Serikali kuendelea na mpango huo.
Hata hivyo mlengwa mwingine Said Mapepe alisema,walengwa wamekuwa wakitoa fedha kwa ajili ya kujiunga na mfuko wa afya ya jamii(CHF)lakini baadhi yao bado hawajapa kadi za matibabu hivyo kupata usumbufu pindi wanapofika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
“walengwa tunatoa fedha kwa ajili ya kujiunga na CHF,lakini tangu tulipoanza kuchangia mwaka 2020 hatujapata kadi zetu za matibabu”alisema Mapepe
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa kijiji cha Chiwana Issa Simba amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kueleza kuwa,wanaohusika ni waratibu wa CHF ngazi ya wilaya na mkoa ambao ndiyo wanaokusanya fedha kutoka kaya maskini.
Simba,amewakumbusha wakazi wa kijiji hicho kuweka akiba ya chakula kwa ajili ya matumizi ya familia zao ili kuepuka kukumbwa na janga la njaa.