KUTOKANA na uharibifu wa vyanzo vya maji na uoto wa asili uliofanyika kandokando ya mto Mbarali uliotokana na shughuri za kilimo na ufugaji mradi wa Eflows unatarajia kuanzisha vitaru vya miti Rafiki kwa mazingira zaidi ya laki moja kwaajili ya kupanda kandokando ya mto huo.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Kiongozi wa mradi huo Prof. Japheti Kashaigili kufanya ziara kandokando ya mto huo akiwa ameambatana na kiongozi wa bonde la mto Rufiji, Jumuiya za watumia maji na Viongozi wa skimu ya umwagiliaji ya Igomelo kwa lengo la kwenda kufanya tathimini ya hali ya mazingira kutokana na shughuri za kilimo na ufugaji.
“Mradi pamoja na kufanya utafiti lakini pia tunataka kuwa sehemu ya kutatua baadhi ya changamoto na kutokakana na hali ilivyo mbaya kwenye vyanzo vya maji vya mto huu na kandonkando ya mto hatua ya kwanza tunaanzisha vitalu vya miti ili ipandwe kwenye maeneo yote baada ya kupata ushauri wa aina ya miti inayofaa kutoka kwa wenzetu wa Wakala wa huduma za misitu Tanzania TFS Wilayani Mbarali” Alisema Prof. Kashaigili.
Aliongeza “Hatuwezi kusubiria hadi mwisho wa utafiti wetu ndio tufanya kazi hii ya kurekebisha makosa ambayo yanaonekana waziwazi hivyo lazima tupande miti rafiki ili kurudisha uoto wa asili maana mto umevuliwa kabisha kwenye maeneo mengi kitu ambacho sio kizuri katika kulinda mto”.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Skimu ya umwagiliaji ya Igomelo Bi. Aurelia Kayombo amemshukuru Mkuu wa Mradi huo kwanza kwa kufanya ziara hiyo kwa pamoja na kuwapatia elimu kuhusu sharia za mazingira na uhifadhi wa mito lakini pia kwa kuamua kuanzisha vitalu hivyo ambavyo vitasaidia kupata miche ya miti rafiki kwaajili ya kupanda kwenye vyanzo vya maji.
“Ziara hii imekuwa ya mafanikio makubwa na nikiri kuwa kuna uharibifu mkubwa umefanyika hatukuwa tunafahamu lakini kupitia ziara hii tumeweza kuona na sasa tunakwenda kuitisha kikao na wananchama wetu wote na kufanya ziara kama hii na ikiwezekana na Viongozi wa wilaya nao wawepo ili tuweke makubaliano ambayo yatasaidia kulinda mto huu muhimu” Alieleza Mwenyekiti huyo wa skimu ya umwagiliaji ya Igomelo.
Aliongeza “Kwakweli lazima tuwe makini sana katika kulinda mto huu maana kwa sasa tunatamba kwakuwa maji yapo na tunalima ila kama hali ya uharibifu itaendelea hivi maana yake hatutaweza kulima,kuishi wala kufuga tena maana hatutakuwa na maji haya tena kwahiyo lazima tuchukue hatua za makusudi sasa”.
Nae mwenyekiti wa jumuiya ya watumia maji wa Mto Mbarali (JUWAMBA) Bw. Siasa Shabani amesema kuwa wamefanya kazi kubwa katika kutoa elimu na kuwakamata watu ambao wamekuwa wakivunja sharia na taratibu walizojiwekea ili kupunguza idadi ya watu wanaoharibu vyanzo vya maji lakini tatizo bado linaendelea.
“Mimi napendekeza kuwepo na sharia kali kwa watu wanaokamatwa kwa kuvunja sharia maana tunamkamata mtu unampeleka kwenye vyombo vya dola na mahakamani lakini faini wanazolipa ni ndogo sana kiasi kwamba hazimpi fundisho ili asirudie tena bali wanazilipa na kurudi kufanya uharibifu sasa kwa mtindo huu hatutaweza kukomesha changamoto hii” Alileza Bwana Siasa.
Akizungumza kwa niaba ya Bodi ya maji ya Bonde la Mto Rufiji katika kidakio cha Mto Ruaha Mkuu Rujewa bwana Abisai Chilunda amesema kuwa bonde la mto mbarali vyanzo vyake vinatokea katika maeneo ya Wilaya ya Wanging’ombe na juhudi kubwa walizozifanya ukiachia mbali swala la elimu pia wameanzisha jumuiya hizo za watumia maji ili zisaidie kusimamia sharia za uhifadhi wa mito.
Amesema Changamoto kubwa iliyopo ni kilimo ndani ya mita sitini za mto,ufugaji na ulishaji mifugo mtoni na kandokando ya mito pamoja na ukataji miti na uchomaji miti iliyo pembezoni mwa mto huo.
“Hivi karibuni Bodi ya Bonde la Mto Rufiji inatarajiwa kuajiri walinzi wa mito na vyanzo vya maji na ninaamini kwa kupata walinzi hawa watasaidia sana juhudi zilizopo katika kulinda mito yetu na hivyo kuweka mazingira salama kwa ustawi wa mito” Alifafanua Bwana Abisai.
Mradi huo wa miaka Miwili unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi ya mazingira (NEMC) unalenga kufanya utafiti kuangalia afya ya mto na kuja na matokeo ya kina ya kisayansi na mapendekezo ambayo yatatakiwa kusimamiwa na kutekelezwa na wadau wote ili pia zitumiwe katika maeneo mengine ya aina hiyo nchini.