Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. George Simbachawene, pamoja na Naibu wake wakiwa katika picha ya pamoja na Makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora walioambatana na Mtendaji Mkuu wa Tume hiyo mara baada ya kumtembelea Ofisini kwake leo tarehe 24 Januari, 2022.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata muda mfupi mara baada ya kumaliza kikao alipomtembelea ofisi kwake leo kwa lengo la kujitambulisha na kumueleza namna Ofisi hiyo inavyotekeleza majukumu yake. Wa pili kushoto ni Wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata akifuatiwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Nalija Luhende na wapili kulia ni Naibu Waziri Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Geofrey Mizengo Pinda akifuatiwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Khatibu Kazungu.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. George Simbachawene, akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Bw. Sylvester Mwakitalu mara baada ya kumtembelea Ofisini kwake leo tarehe 24 Januari, 2022. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Haki za Binadamu.
************************
Na: Dennis Buyekwa – OSG.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. George B. Simbachawene, leo tarehe 24 Januari 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya Viongozi kutoka Taasisi zilizoko chini ya Wizara hiyo kwa lengo la kutaka kufahamu namna ofisi hizo zinavyotekeleza majukumu yake.
Akizungumza na viongozi hao kwa nyakati tofauti Mhe. Simbachawene amewashukuru Viongozi hao kwa kumtembelea ofisini kwake huku akiwasihi viongozi hao kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili wote kwa pamoja waweze kufikia malengo waliyojiwekea.
Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa ni muhimu kwa kila Taasisi iliyoko chini ya Wazara yake kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwani kwa kufanya wataisaidia serikali kuharakisha maendeleo kwa wananchi wake kupitia sekta ya sheria.
“Kila Taasisi ni vyema ikatekeleza majukumu yake kwa mujibu ya sheria, taratibu na kanuni ili tuweze kuisaidia serikali kuwaletea maendeleo wananchi kupitia sekta ya sheria.” Alisema Simbachawene.
Aidha Mhe. Waziri ameahidi kuzichukua na kuzifanyia kazi changamoto zote zilizowasilishwa na Viongozi hao hatua itakayoongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku mara tu zitakapotatuliwa.
Wakieleza changamoto zinazowakabili wamezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni ufinyu wa bajeti, ukosefu wa vitea kazi kama vile umiliki wa majengo ya ofisi, Magari, upungufu wa watumishi pamoja na kutokuwa na kompyuta za kutosha kwa ajili ya kutumia ipasavyo mifumo ya TEHAMA hususani kwa zile Taasisi zinazohusika na uendeshaji wa Mashauri ya Serikali.
Naye Naibu Waziri Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Geofrey Mizengo Pinda, amewapongeza viongozi hao kwa kufanya kazi kwa bidii na kuahidi kuendelea kuwa kiungo muhimu kati ya Taasisi hizo na Wazara ili kuhakikisha Taasisi hizo zinatimiza malengo yao waliyojiwekea kulingana na mpango kazi wa Taasisi zao.
Kwa upande wao viongozi hao wakiongea mara baada ya kumalizika kwa Kikao kazi hicho wamemshukuru Mhe. Waziri kwa kukubali kukutanao naoi li waweze kuzungumza ambapo viongozi hao wametumia fursa hiyo kumuuleza majukumu ya ofisi zao na namna wanavyoyatekeleza.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Katiba na Sheria uliopo Mtumba Jijini Dodoma, kimewahusisha Viongozi wa Tasisi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.