………………………………………………
Na John Walter-Hanang
Waziri Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa ametoa wiki mbili kwa Bohari ya Dawa (MSD) ihakikishe ifikapo Februari 5, 2022 iwe imeshafikisha vifaa vyote vinavyohitajika katika vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Manyara kwa kuwa tayari fedha zimeshalipwa.
“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa maagizo kuwa vituo vyote vya afya vinapokamilika vianze kutoa huduma, hivyo MSD lazima ihakikishe inafikisha vifaa katika vituo hivyo haraka. Majengo ya kutolea huduma yameshakamilika tunataka tuone yakitumika na yasipotumika yataharibika.”
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Januari 23, 2022 alipokagua mradi ya ujenzi wa kituo cha afya cha Mogitu kilichopo wilayani Hanang’ akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali mkoani Manyara.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya nchini, hivyo kukamilika kwa kituo hicho cha afya cha Mogitu kunalenga kusogeza huduma za afya kwa wananchi na kuwapunguzia kutembea umbali mrefu wa kufuata huduma hizo katika kituo cha afya cha Kata ya Katesh.
Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mganga Mkuu wa wilaya ya Hanang Dkt. Boniface Manditi ahakikishe kituo hicho kianzaa kutoa huduma za afya kwa wananchi kwa kuwa tayari ujenzi wake umekamilika.
Naye Mganga Mkuu wa wilaya ya Hanang’ Dkt. Manditi amesema gharama za utekelezaji wa mradi huo ni sh. milioni 578,926,000 ambapo kati yake sh. milioni 400 zimetolewa na Serikali Kuu, sh. milioni 125,726,000 zimetolewa na Halmashauri ya Hanang’ na mchango wa wananchi ni sh. milioni 53,200,000. Dkt. Manditi amemuhakikishia Waziri Mkuu kuwa kuanzia kesho Jumatatu Januari 24, 2022 huduma zitaanza kutolewa kituoni hapo.
Amesema kituo hicho kinatarajiwa kuhudumia jumla ya wakazi 11,725 kutoka katika vijiji vitatu vya kata ya Mogitu ambavyo ni Mogitu, Gabadaw, Gidagamowd na wakati wa maeneo ya jirani. Amesema mradi huo uko katika hatua za ukamilishaji ukiwemo ukamilishaji wa mifumo ya maji safi na maji taka.