Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akizungumza
katika mkutano wa hadhara na maelfu ya Wakimbizi wa Kambi ya
Nduta (hawapo pichani) Wilayani Kibondo, Mkoani Kigoma, leo.
Lugola aliambatana na Waziri wa Mambo ya Ndani kutoka nchini
Burundi, Pascal Barandagiye, ambapo walitembelea katika Kambi za
Nduta na Mtendeli mkoani humo, kwa lengo la kuhamasisha
wakimbizi kurejea nchini mwao kwa hiari. Picha na Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani na Elimu ya Uzalendo, Pascal
Barandagiye akizungumza katika mkutano wa hadhara na maelfu ya
Wakimbizi wa Kambi ya Nduta (hawapo pichani) Wilayani Kibondo,
Mkoani Kigoma, leo. Waziri huyo aliwaambia Wakimbizi hao, warudi
nchini mwao kwa kuwa sasa nchi hiyo ina amani na ipo tayari
kupokea wakimbizi hao waliopo nchini. Lugola aliambatana na Waziri
huyo kutembelea Kambi za Nduta na Mtendeli mkoani humo, kwa
lengo la kuhamasisha wakimbizi kurejea nchini mwao kwa hiari.
Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akizungumza
katika Kikao kilichoshirikisha pande tatu, Serikali ya Tanzania,
Burundi na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR),
kilichofanyika katika Kambi ya Wakimbizi ya Nduta, Wilayani Kibondo,
Mkoani Kigoma, leo. Kikao hicho kilikua na lengo la kuhamasisha
Wakimbizi wa Burundi warejee nchini mwao kwa hiari. Watatu
kushoto ni Waziri wa Mambo ya Ndani kutoka nchini Burundi, Pascal
Barandagiye. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa
Wakimbizi nchini, Sudi Mwakibasi. Picha na Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto),
akipokelewa na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi
nchini, Sudi Mwakibasi, wakati alipokuwa anawasili katika eneo la
mkutano wa hadhara, Kambi ya Nduta, Wilaya ya Kibondo Mkoani
Kigoma, leo. Lugola aliambatana na Waziri wa Mambo ya Ndani
kutoka nchini Burundi, Pascal Barandagiye, ambapo walitembelea
katika Kambi za Nduta na Mtendeli mkoani humo, kwa lengo la kuhamasisha wakimbizi kurejea nchini mwao kwa hiari. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Sehemu ya Wakimbizi wa Burundi wakimshangilia Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (hayupo pichani), alipokuwa
anazungumza na maelfu ya wakimbizi hao, katika Kambi ya Nduta,
Wilayani Kibondo, Kigoma, leo. Lugola aliambatana na Waziri wa
Mambo ya Ndani kutoka nchini Burundi, Pascal Barandagiye, ambapo
walitembelea katika Kambi za Nduta na Mtendeli mkoani humo, kwa
lengo la kuhamasisha wakimbizi kurejea nchini mwao kwa hiari.
Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
********************
Na Felix Mwagara, Kibondo (MOHA).
Baadhi ya Wakimbizi kutoka nchini Burundi wanaoishi katika Kambi ya
Nduta, Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma wamesema wanawekewa
vikwazo na kucheleweshwa na baadhi ya watendaji wa mashirika ya
wakimbizi kambini humo wakati wanapoomba kujiandikisha kurejeshwa
kwao.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola na Waziri wa Mambo ya Ndani na
Elimu ya Uzalendo kutoka nchini Burundi, Pascal Barandagiye, wakimbizi
hao wamesema wapo tayari kurudi nchini mwao kwa hiari lakini
wanashindwa kujiandikisha kutokana na kukwamishwa na baadhi ya
watendaji wa mashirika hayo.
Mkimbizi wa kambi hiyo, Nzoisa Bhainoje, alisema yupo tayari kurejea
nchini Burundi lakini amefanya juhudi za kwenda eneo la kujiandikisha
kambini hapo lakini hakufanikiwa kutokana na kusumbuliwa akiambiwa
kuwa idadi wanaotakiwa kuondoka imekamilika.
“Nakumbuka nilifika eneo la kuondoka siku ya Jumanne lakini ilishindikana
kujiandikisha kutokana na kukwamishwa, wengi tunataka kuondoka lakini
tunashindwa kuondoka kwasababu tunakwamishwa,” alisema Bhainoje.
Bhainoje aliongeza kuwa, wanaomba watendaji hao wawaruhusu kwa wale
wanaotaka kurejea nchini mwao kwa hiari, lakini kwa wale ambao hawataki
kuondoka wanaweza kubaki kwa mipango yao.
Baada ya wakimbizi hao kutoa kero zao kwa Waziri Lugola na Waziri
Barandagiye, ndipo Lugola aliagiza kufanyika uchunguzi katika kambi hiyo kuwakamata wale wote ambao wanakwamisha wakimbizi hao kurejea nchini kwao kwa hiari.
“Naagiza uchunguzi ufanyike haraka iwezekanavyo kwa yeyote
atakayehusika anakwamisha zoezi hili la kuwarejesha wakimbizi hawa
ambao wapo tayari kuondoka nchini kwao kutokana na amani iliyopo, awe
Afisa kutoka Wizarani, awe afisa wa shirika lolote, awe yupo hapa kambini,
lazima tutamkamata na kumpeleka mahakamani,” alisema Lugola.
Aliongeza kuwa, muda umefika kwa wakimbizi wa Burundi kurudi nchini
mwao, kwasababu zile sababu ambazo zilikuwa zinazuia zoezi la
kuwarudisha kwao wakimbizi hao kwa sasa havipo tena kwasababu nchi
hiyo ina amani.
Alisema Serikali ya Tanzania chini ya Rais John Magufuli imejiridhisha
sababu kubwa iliyowaleta wakimbizi hao wa Burundi nchini ya kutowepo
kwa amani haipo tena na kwamba kwa sasa Burundi ipo salama kiulinzi na
kiusalama pia kisiasa hivyo wakimbizi hao wanapaswa kurudi nchi mwao
wote bila kuwepo kikwazo chochote.
“Wanaosema Burundi haina amani wanaipaka matope nchi hiyo kwani
jambo hilo halina ukweli wowote na Tanzania imefanya uchunguzi wa
kutosha na kujiridhisha kuwa amani ya kudumu ipo nchini humo, Oktoba
Mosi tutaanza kutekeleza mkataba wa pande tatu wa kurudishwa kwa
wakimbizi 2000 kila wiki wa Burundi kwenda nchini mwao”. Alisema Lugola.
Naye Waziri Barandagiye, kwa upande wake alisema Burundi iko tayari
kutekelezwa kwa makubaliano ya pande tatu ya kuhakikisha wakimbizi
wote wa Burundi wanaohifadhiwa kwenye makambi mbalimbali ya
wakimbizi mkoani nchini wanarudi Burundi lakini wanashangazwa na
namna Shirika la Kuhudumia Wakimbizi linavyoendesha zoezi hilo kwa kasi
ndogo.
"Tuko tayari kupokea wakimbizi 3000 kila wiki zaidi ya takwimu ya
wakimbizi 2000 iliyotolewa kwenye makubaliano ya pande tatu, maandalizi
na matayarisho ya kupokea wakimbizi hao yapo vizuri na wengi wanaorudi wamekuwa wakipata misaada mbalimbali ikiwemo miradi ya kiuchumi kwa ajili ya kuendesha maisha yao,"Alisema Barandagiye.
Barandagiye amewataka wakimbizi hao kutokubali kudanyanywa na
maneno ya wanasiasa kwamba hakuna amani nchini Burundi lakini kuwa
na tamaa ya kwenda kuishi Marekaani, Canada kuwa huo ni uongo hivyo
wqanapaswa kurejea nchini mwao kwakuwa ipo amani na pia mazingira
yanaruhusu kuppokelewa.
Waziri Lugola na Barandagiye walitembelea Kambi ya Nduta, Wiliyani
Kibondo na Mtendeli iliyopo Wilayani Kakonko mkoani humo, kwa lengo la
kuhamasisha wakimbizi katika kambi hizo kurejea nchini kwao kwa hiari.