Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Idara ya Ujenzi Balozi, Mhandisi. Aisha Amour (wa tatu kutoka kulia) akiwa na Watendaji wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) jijini Dar es Salaam wakati akikagua Nyumba za Magomeni Kota.
Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Idara ya Ujenzi Balozi, Mhandisi. Aisha Amour (wa tatu kutoka kulia) akipewa maelekezo ya mradi na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Daud Kondoro (wa kwanza kutoka kushoto).
Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Idara ya Ujenzi Balozi, Mhandisi. Aisha Amour akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya kufanya ukaguzi wa mradi wa Magomeni Kota.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Daud Kondoro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa nyumba za Magomeni Kota (Picha zote na Noel Rukanuga
……………………………………………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Idara ya Ujenzi Balozi, Mhandisi. Aisha Amour amewataka wananchi wote wanaotarajia kuishi katika nyumba za makazi Magomeni Kota kutunza miundombinu za nyumba hizo jambo ambalo litasaidia serikali kuendelea kufanya maboresho ya makazi katika maeneo mbalimbali nchini.
Ujenzi wa nyumba za makazi Magomeni Kota umekamilika kwa asilimia mia moja, huku ikitegemewa kuhamia wakazi 644 waliokuwa wakiishi katika makazi hayo, kabla ya Serikali kufanya ujenzi wa makazi hayo ya kisasa yakihusisha huduma muhimu ikiwemo maduka na Soko.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaama baada ya kufanya ukaguzi wa mradi wa magomeni Kota, Balozi Mhandisi. Aisha amesema kuwa wakati wowote wananchi watahamia katika nyumba za magomeni kota na kuanza kuishi.
“Baada ya kutembelea nyumba kwa ufuatiliaji nmejiridhisha kazi imekamilika na maboresho madogo madogo yamefanyika na muda wowote kuanzia sasa wakazi halali watahamia katika nyumba hizo na kuishi kama Serikali ilivyoahidi” Mhandisi. Amour
Amesema uwekezaji huo uliofanywa na Serikali ni mkubwa hivyo wakazi wa nyumba hizo lazima walinde miundombinu ya nyumba ili kuipunguzia gharama serikali kwa kufanya marekebisho.
Ameeleza kuwa miundombinu yote ipo salama na imara, wakazi watakaoishi ni vyema wakaitunza miundombinu ili serikali itumie fedha kuendelea kuboresha makazi ya wananchi.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Daud Kondoro amesema kuwa kuna familia 644 wanaotarajiwa kuishi magomeni kota na uhakiki umekamilika.
”Ufungaji wa lift kumi zitakazotumika katika majengo haya umekamilika, kuna sehemu ya uwekezaji wa maduka sakafu mbili unaendelea, kuna vizimba 186 katika uwekezaji wa soko pamoja na vyoo vya kulipia.” Amesema Arch. Kondoro.
Amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo umezingatia viwango vya hali ya juu na rasilimali za tofali na zege iliyotumika katika ujenzi huo ni zao la kiwanda kilichopo katika makazi hayo chini ya Wakala hiyo.
Amesema kuwa wamefanya ziara ya ufatiliaji ambapo kazi imekamilika na wakati wowote wananchi wanataruhusiwa kuingia katika nyumba na mradi utafunguliwa.