Naibu Waziri Kilimo Anthony Mavunde akizungumza na watendaji wa Bodi ya Sukari wakato alipofanya ziara katika Bodi hiyo jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Kilimo Anthon Mavunde akiangalia ramani ambayo inaonyesha maeneo yanayoweza kuwekezwa kwa kilimo cha Miwa na kufanya kuwa sukari ya kutosha nchini wakati alipofanya ziara Bodi ya Sukari jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri Anthony Mavunde akizungumza na watendaji wa Bodi ya Sukari wakato alipofanya ziara katika Bodi hiyo jijini Dar es Salaam.
***************
Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde* ameitaka Bodi ya Sukari kuhakikisha inasimamia kwa weledi mpango mkakati wa kuwawezesha wakulima wadogo kuzalisha miwa kwa tija.
Mhe Mavunde ameyasema hayo leo tarehe 22 Januari, 2022 Jijini Dar es Salaam alipofanya ziara ya kutembelea Bodi ya Sukari Tanzania.
Bado tunayo fursa kubwa ya kuwatumia wakulima wadogo katika kuongeza uzalishaji wa miwa nchini kwa kuwaunganisha na Taasisi za fedha, kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji na kuwakusanya katika vikundi na kuwahamasisha kuanzisha viwanda vidogo vya kuzalisha sukari
Kwa sasa tija ya uzalishaji wa miwa kwa wakulima wadogo ni wastani wa tani 47 kwa hekta, wakati wakulima wakubwa ni wastani wa tani 87 kwa hekta. Hivyo, tunalo jukumu la kuhakikisha tunawasimamia wakulima wadogo wa miwa kuongeza tija ili waweze kupata kipato zaidi”, Alisema Mhe Mavunde.
Aidha, Mhe. Mavunde aliwataka watumishi wa Bodi ya Sukari kuwa wabunifu katika utendaji kazi wa majukumu yao na kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kutumia ujuzi na maarifa yao kuishi maono ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza tasnia ya sukari nchini.
Akitoa maelezo ya awali Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Prof. Kenneth Bengesi amemueleza Naibu Waziri Mavunde kwamba Bodi imejipanga kuhakikisha kwamba inawasimamia wakulima wa miwa nchini kuongeza tija katika kilimo kwa kusimamia upatikanaji wa mbegu safi,kuboresha miundombinu ya umwagiliaji na kuwaunganisha na Taasisi za Fedha nchini.