Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akizungumza na wanafunzi wa Shule ya awali katika Kiwanda cha Sukari mkoani Kagera, alipotembelea shule hiyo.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akimsikiliza Mhandisi Umwagiliaji Neema Senyael wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera, alipokagua miundombinu ya kiwanda hicho.
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya daraja la Kitengule lenye urefu wa Mita 40 linalounganisha Wilaya za Misenyi na Karagwe, mkoani Kagera.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akisisiza jambo kwa Wasimamizi wa ujenzi wa Daraja la Kitengule lenye urefu wa mita 40 alipokagua maendeleo ya ujenzi wake mkoani Kagera.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akiangalia mtambo wa kuunganisha mabomba katika shamba la Miwa la kiwanda cha sukari cha Kagera.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akishuka katika moja ya magari yanayotumika kuandaa mashamba ya miwa katika kiwanda cha sukari Kagera, alipokagua miundombinu ya barabara katika kiwanda hicho.
…………………………………………………………….
Imeelezwa kuwa kufanikiwa kwa miradi ya kiuchumi na uzalishaji katika mkoa wa Kagera kutategemea kukamilika kwa haraka kwa miundombinu ya barabara na madaraja mkoani humo.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema hayo alipokagua ujenzi wa daraja la Kitengule lenye urefu wa mita 140 na barabara unganishi za daraja hilo zenye urefu wa KM 18.
Amesema kukamilika kwa darala hilo na barabara unganishi kutahuisha shughuli za kilimo, biashara na kuongeza uzalishaji wa sukari katika kiwanda cha Kagera.
“Kutokana na kazi kubwa inayofanyika hapa ya ujenzi wa daraja na barabara ni Dhahiri kutachangia uzalishaji mkubwa wa miwa na mazao mengine ya kilimo hivyo nakuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Kagera kuanza usanifu wa barabara hii sehemu iliyobaki ya Kitengule-Bunazi KM 24 ili kuziunganisha Wilaya za Misenyi na Karagwe kwa lami’ amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Amekipongeza kiwanda cha sukari cha Kagera kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya maji itakayokiwezesha kuongeza uzalishaji wa sukari nchini.
Naye Meneja TANROADS mkoa wa Kagera Eng. Yudas Msangi amesema ujenzi wa daraja la Kitengule umesanifiwa kupitisha uzito wa tani mia moja na kwa sasa umefikia asilimia 90 kukamilika na barabara unganishi zenye urefu wa KM 18 zinatarajiwa kukamilika mwezi mei mwaka huu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Sukari Kagera Bw. Seif Seif amesema Ujenzi wa daraja la Kitengule lenye urefu mita 40 na barabara unganishi zenye urefu wa KM 18 zinazounganisha Wilaya ya Misenyi na Karagwe ukikamilika utarahishisha kazi ya uzalishaji wa sukari katika kiwanda hicho na kuibua fursa nyingi za ajira ambapo tumejipanga kuongeza ukubwa wa mashamba ili kutatua changamoto ya upungufu wa sukari nchini.
Aidha, ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa barabara katika Wilaya za Misenyi na Karagwe na kusisitiza kwamba kiwanda hicho kitatoa ushirikiano wote unaohitajika katika kuhakikisha malengo ya Serikali katika kuongeza uzalishaji wa sukari, kutoa ajira kwa wahitimu wa kada zinazohitajika katika kiwanda hicho yanafikiwa kwa wakati.
Amesema kwa sasa kiwanda kinazalisha sukari tani elfu tisini na nne ila kutokana na kukamilika kwa miundombinu na daraja la Kitengule kunatoa fursa ya kuongeza mashamba na katika miaka mitatu ijayo kiwanda kimejipanga kuzalisha tani 170,000/- kwa mwaka.
Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Kanali Wilson Sakulu ameipongeza Serikali kwa kuziunganisha Wilaya ya Misenyi na Karagwe kwa barabara ya lami na daraja la uhakika kwani kutainua uchumi na kuongeza usalama kwa wakazi wa Wilaya hizo.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa yuko katika ziara ya siku tatu kukagua maendeleo ya miradi ya Sekta ya Ujenzi na Uchukuzi na kuhamasisha wadau wa mbalimbali kuibua fursa za uchumi mkoani Kagera.