* Ipo ya Stadi za Maisha kwa kuzingatia Afya ya Uzazi, VVU/UKIMWI, Jinsia na kuhusiana na kwa Heshima
* UNESCO yatoa mchango mkubwa wa Fedha, Utaalam
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO,) limekabidhi Miongozo ya Kufundishia Elimu ya Stadi za Maisha kwa kuzingatia Afya ya Uzazi, VVU/UKIMWI, Jinsia na Kuhusiana kwa Heshima kwa Walimu na Shule za Msingi na Sekondari kwa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET,) ikiwa ni jitihada katika kuboresha sekta ya elimu pamoja na kujenga kizazi cha vijana wanaojitambua na kufanya maamuzi bila kukatiza ndoto zao.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya miongozo hiyo iliyofanyika leo katika ofisi za TET jijini Dar es Salaam Kamishina wa Elimu Tanzania kutoka Wizara ya Elimu, Sanyansi na Teknolojia Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema, miongozo hiyo inafafanua kwa kina jinsi ya kujenga umahiri na maudhui ya Afya ya Uzazi, VVU na UKIMWI pamoja na Elimu ya Jinsia kama ilivyoainishwa katika mihtasari ya Elimu ya Msingi na Sekondari.
”Miongozo hii kama itatumika kwa usahihi itasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi hizo za elimu na kujenga Taifa lenye vijana imara.” Amesema.
Dkt. Mtahabwa ameishukuru na kuipongeza Taasisi ya Elimu Tanzania kwa kusimamia na kutekelezwa kwa ufanisi uandishi wa miongozo hiyo, na kulishukuru kwa dhati Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO,) kwa mchango wake mkubwa wa kifedha na kitaalam katika kufanikisha uandaaji wa miongozo hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wakiwemo Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS,) na Marie Stopes Tanzania ambao kwa kiasi kikubwa wameshiriki mchakato wa uandaaji wa miongozi hiyo.
Aidha amewataka walimu kote nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya kazi na kuuweka upendo mbele kwa wanafunzi wanaowafundisha.
”Kama mwalimu huna upendo ni bure, Mwanafunzi aanze kukupenda wewe na namna unavyohusiana na wenzako ofisini, unavyovaa bila kutanguliza ubabe, dharau na dhihaka kwa wanafunzi,,,,Tuwapende ili tuweze kuwasaidia.” Amesema.
Vilevile amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI wataendelea kusimamia na kuratibu matumizi ya miongozo hiyo na kwa kushirikiana na wadau wataendelea kudurufu na kusambaza miongozo hiyo ili iweze kupatikana kwa urahisi na kutoa fursa kwa wadau wengine kupata nakala hizo na kuzitumia katika kutoa elimu iliyokusudiwa.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkuu wa Ofisi ya UNESCO Kanda ya Mashariki Prof. Hubert Gijzen amesema UNESCO imekuwa ikishirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo elimu na kupitia miongozo hiyo wanafunzi watanufaika na maarifa yatakayowasaidia katika masuala ya afya ya uzazi, ukatili wa kijinsia, stadi za maisha na masuala ya VVU na UKIMWI.
Amesema UNESCO itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha na kuinua sekta muhimu ya elimu ili kuinua kiwango cha elimu kwa kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji.
”UNESCO imeshirikiana na TET tumefanikisha kwa kiasi kikubwa kuwa na nakala nyingi za miongozo hii itakayotumika katika shule zetu ambayo italeta matokeo chanya katika sekta ya elimu.” Amesema.
Prof. Hurbet amesema miongozo hiyo ilifanyiwa marekebisho kwa mara ya mwisho mwaka 2013 na mabadiliko yaliyofanywa yanakwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia hasa katika masuala ya tiba na mabadiliko hayo yamezingatia mila, desturi na maadili ya kitanzania.
Awali akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Mkurugenzi wa Mafunzo ya Mitaala Dkt. Fika Mwakabungu amesema kuwa Taasisi hiyo imeshiriki mchakato huo wa kusimamia uandishi wa miongozo hiyo ili kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga vijana wanaojitambua na kufanya maamuzi bila kukatisha ndoto zao.
Dkt. Fika amesema Serikali imefanya jitihada kubwa katika kujenga na kuboresha miundombinu ya elimu ya elimu ikiwemo madarasaa, samani, na vitabu na jukumu la walimu ni kuwapenda na kuwaelimisha wanafunzi ili kufikia lengo la kutoa elimu bora pamoja na kutokomeza kabisa vitendo vya unyanyasaji, mimba za utotoni na magonjwa ukiwemo UKIMWI.
Hafla hiyo imehudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo maafisa kutoka UNESCO, TET, TACAIDS, Marie Stopes, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Maafisa elimu wa Mkoa na Wilaya, wadau wa elimu, walimu na wanafunzi.
Kamishina wa Elimu Tanzania kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Lyabwene Mtahabwa akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya miongozo hiyo na kuwataka walimu kuwa na upendo pindi wanapowahudumia wanafunzi.
Mwakilishi na Mkuu wa Ofisi ya UNESCO Kanda ya Afrika Mashariki Prof. Hubert Gijzen akizungumza wakati wa makabidhiano ya Miongozo ya Kufundishia Elimu ya Stadi za Maisha kwa kuzingatia Afya ya Uzazi, VVU/ UKIMWI, Jinsia na Kuhusiana kwa Heshima kwa walimu wa shule za msingi na sekondari na kueleza kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha sekta ya elimu.
Mkurugenzi wa Idara ya Mwitikio wa Kitaifa wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS,) Audrey Njelekela akizungumza wakati wa makabidhiano ya miongozo hiyo na kueleza kuwa miongozo hiyo italeta ufahamu zaidi kwa wanafunzi kupata maarifa ya kujitambua na kufanya maamuzi ambayo hayataathiri wala kukatiza ndoto zao.
Mkurugenzi wa Marie Stopes Tanzania, V.S Chandrashekar akizungumza wakati wa kukabidhi miongozo hiyo na kuipongeza TET kwa kuandaa miongozo hiyo na kuwashirikisha katika mchakato huo wa kuinua kiwango cha elimu Tanzania kupitia miongozo hiyo.