Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (wa pili kushoto) akiagiza Wakaguzi wa Ndani nchini kukagua fedha za miradi ya maendeleo zilizotolewa na Serikali katika maeneo yao na kuwasilisha taarifa ndani ya mwezi mmoja, wakati akizungumza na wananchi wa Mji Mdogo wa Mwandiga, mkoani Kigoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akimsikiliza Mzee wa Mji Mdogo wa Mwandiga Mkoani Kigoma, baada ya Mkutano wake na Wananchi wa eneo hilo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani hapo.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Mhe. Assa Makanika, akieleza kero za wananchi wa jimbo hilo kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipotembelea mji mdogo wa Mwandiga, Mkoani Kigoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (wa kwanza kushoto) akipiga ngoma na Mwananchi wa Mji Mdogo wa Mwandiga Mkoani Kigoma kabla ya Mkutano na Wananchi wa eneo hilo.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akisikiliza maelezo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Bi. Rose Manumba, kuhusu utekelezaji wa Ujenzi wa Kituo cha Afya katika Mji Mdogo wa Mwandiga, Mkoani Kigoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akisikiliza kero kutoka kwa wananchi wa Mji Mdogo wa Mwandiga Mkoani Kigoma, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Mji huo.
Wananchi wa Mji Mdogo wa Mwandiga Mkoani Kigoma, wakimsikiliza Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (hayupo pichani) alipokuwa akitoa maelekezo kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kuhusu kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wakati.
Picha na Saidina Msangi, WFM, Kigoma
************************
Na. Peter Haule na Saidina Msangi, WFM, Kigoma
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amewaagiza Wakaguzi wa Ndani nchini kukagua fedha za miradi yote ya maendeleo zilizotolewa na Serikali katika maeneo yao na kuwasilisha taarifa ndani ya mwezi mmoja.
Maagizo hayo aliyatoa mji mdogo wa Mwandiga alipokutana na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Kigoma.
Dkt. Nchemba aliagiza wakaguzi wa ndani wakague fedha zote zilizotolewa katika maeneo yao wakiainisha miradi iliyotekelezwa, kiwango cha utekelezaji wa miradi na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji na thamani ya miradi hiyo.
“Wakaguzi wa Ndani nchi nzima ndani ya mwezi mmoja mniletee taarifa inayoainisha fedha iliyopokelewa, imetumika kwa kiwango gani, kiwango cha ukamilishaji wa miradi na kiwango cha ubora na pia kama mradi haujatekelezwa kabisa au umetekelezwa hovyo mniambie, na wale waliofanya kazi hiyo taarifa itatuambia kama wana uwezo kiasi gani wa kufanya kazi hiyo”, alieleza Dkt. Nchemba
Alisema kuwa kwa upande wa miradi ya Vituo vya Afya, Serikali inatarajia kutoa fedha kwa awamu ya pili kiasi cha shilingi milioni 250 ili kufikia jumla ya kiasi cha shilingi milioni 500 mwishoni mwa mwezi Februari kwa ajili ya kukamilisha miradi ya vituo vya afya inayoendelea lakini kabla ya kutoa fedha hizo ni lazima Serikali ipate taarifa ya kazi iliyofanyika kulingana na thamani ya fedha iliyotolewa.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali haitavumilia mtumishi yeyote atakayechelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo wakati fedha zimetolewa na Serikali kwa wakati na iwapo wakaguzi wa ndani wakishindwa kutoa taarifa sahihi ndani ya mwezi mmoja hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Aidha, alibainisha kuwa kwa sasa Serikali haitarejesha fedha Serikalini kwa sababu ya hati chafu bali itashughulika na wanaosababisha kupatikana kwa hati chafu ambazo zinakosesha wananchi kupata maendeleo.
“Haiwezekani kumuadhibu mwananchi kwa kosa la watu wachache ambao wamepewa jukumu la kufanya kazi kwa niaba ya wengine, hivyo iwapo kutatokea kuwepo kwa hati chafu, watawajibishwa wahusika kwa kuwa mwananchi siyo wanaosababisha hati hizo”, alieleza Dkt. Nchemba
Naye Mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini Mhe. Assa Makanika, alisema kuwa kumekuwa na mvutano kuhusu eneo la ujenzi wa kituo cha afya katika mji mdogo wa Mwandiga na kuelekeza madiwani wa maeneo hayo kutatua changamoto hiyo haraka kabla ya kumalizika kwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa vituo vya afya nchini utaokamilika mwezi Februari, 2022.
Aidha alieleza kero mbalimbali za wananchi ikiwemo barabara, vitambulisho vya Taifa, upatikanaji wa maji pamoja na huduma ya kituo cha polisi ambapo Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Nchemba aliahidi kuziwasilisha katika sekta husika ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.