******************************
Na Mwamvua Mwinyi,Mafia
WAZIRI wa maji, Jumaa Aweso amezindua mradi mkubwa wa maji ,kisiwa cha Jibondo ,Mafia Mkoani Pwani, uliogharimu Bilioni mbili ambapo, unakwenda kuondoa kero ya maji iliyodumu kwa miaka 60 kisiwani humo.
Kutokana na ukosefu wa maji na chanzo cha uhakika ,Serikali ilihangaika chini ya Wakala wa maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kupata ufumbuzi ,na kulazimika kupitisha mabomba ya maji chini ya bahari umbali wa km.7 kutoka Kijiji cha Kiegeani Kitongoji cha Utende .
Akizindua mradi huo ,Aweso alisema haikuwa rahisi kutekeleza na kujenga mradi huo mkubwa kutokana na changamoto zilizokuwepo.
“Lakini Serikali yetu chini ya Rais Samia Suluhu Hassan mradi umekamilka, Tumshukuru Sana ,niwaombe mradi huu muulinde ili uwe historia kwa vizazi vijavyo”alisema Aweso.
Aweso alisema ,baada kukamilika mradi huo Jibondo , Serikali imetoa fedha nyingine Bilioni 4.5 kujenga mradi mwingine wa maji Kilindoni wilayani Mafia.
Hata hivyo ,aliwataka wataalamu wa RUWASA kufanya tathmini ili waweke gharama rafiki kwa wananchi waweze kugharamia na kuweza kunufaika na mradi huo.
Akitoa taarifa ya mradi ,meneja RUWASA Pwani Beatrice Kasimbazi, alieleza wakazi wa Jibondo walitumia maji yaliyovunwa wakati wa msimu wa mvua.
Aidha Kasimbazi alibainisha, ili kukidhi hitaji la maji katika kipindi cha kiangazi,wananchi walilazimika kununua maji kutoka kijiji cha Kiegeani kwa sh.700 hadi 1,500 na kuyasafirisha kwa kutumia vyombo vya baharini kwa umbali wa km.8 na Kisha nchi kavu km .2 .
Vilevile Mkurugenzi Mkuu RUWASA, Clement Kivegalo alieleza mradi huo ni mkubwa na wa kujivunia kwakuwa umeleta tija kwa wananchi waliokuwa wakipoteza muda mwingi kusaka maji kwenda na kurudi umbali wa km.20 .
“Ni mradi ambao RUWASA tunajivunia ,na umetupa uzoefu kufanya miradi mingine mikubwa yenye changamoto ya Aina hii ,alisema Kivegalo.
Awali meneja wa RUWASA Mafia Clement Lyoto alisema ,ujenzi wa mradi ulianza mwaka 2018 ,umetumia bilioni 2 na utanufaisha wakazi 2,050 .
“Mwanzo changamoto iliyokwamisha upelekaji maji kisiwani hapo ilikuwa ni ukosefu wa chanzo cha uhakika “.alisema Lyoto.
Mbunge wa Jimbo la Mafia ,Omary Kipanga na baadhi ya wakazi wa Jibondo waliishukuru Serikali kwa upatikanaji wa maji na umekuwa mkombozi kwao.
Aliishukuru Serikali ya awamu ya sita na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Ruwasa kwa kumtua ndoo Mama kichwani ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) .