Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza wakati akifungua Kikao Kazi cha siku mbili cha Washauri wa Mifugo wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Mifugo na Uvuvi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kinachofanyika jijini Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa wizara za Mifugo na Uvuvi pamoja na Tamisemi mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha siku mbili cha Washauri wa Mifugo wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Mifugo na Uvuvi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kinachofanyika jijini Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akikata utepe wakati wa kukabidhi jumla ya pikipiki 300 kwaajili ya kazi za maafisa ugani katika Halmshauri 140 hapa nchini mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha siku mbili cha Washauri wa Mifugo wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Mifugo na Uvuvi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kinachofanyika jijini Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akijaribu moja ya pikipiki kati ya pikipiki 300 zilizotolewa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwaajili ya kazi za Maafisa Ugani katika Halmshauri 140 hapa nchini mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha siku mbili cha Washauri wa Mifugo wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Mifugo na Uvuvi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kinachofanyika jijini Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka kwa niaba ya wakuu wa mikoa 25 mfano wa ufunguo wa Pikipiki zilizotolewa kwaajili ya kazi za Maafisa Ugani katika Halmashauri 140 hapa nchini mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha siku mbili cha Washauri wa Mifugo wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Mifugo na Uvuvi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kinachofanyika jijini Dodoma.
…………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango,amesema serikali itaendelea kuipa umuhimu Sekta ya Mifugo hapa nchini ili iweze kuwainua wananchi kutoka katika lindi la umaskini kwa kutoa ajira na fursa mbalimbali.
Makamu wa Rais ameyasema hayo leo Januari 17, 2022 wakati akifungua Kikao Kazi cha siku mbili cha Washauri wa Mifugo wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Mifugo na Uvuvi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kinachofanyika jijini Dodoma.
Dkt.Mpango amesema kuwa sekta hiyo huchangia usalama wa chakula, na upatikanaji wa lishe bora pamoja na malighafi katika viwanda vya kuchakata na kusindika mazao ya mifugo hususani viwanda vya nyama, ngozi na maziwa.
“Sekta ya mifugo imejaa fursa. Kila penye mifugo pana chakula, ajira, biashara na kipato kwa wananchi. Hata hivyo, ili sekta ya mifugo iweze kukua, kutoa mchango mkubwa zaidi kwa Taifa na kuwezesha wafugaji na wananchi kwa ujumla kutumia fursa hizo ili kuboresha maisha yao, tunahitaji kuweka msukumo mkubwa katika kuimarisha huduma za ugani na huduma mwambata katika maeneo yafuatayo,” amesema
Dk Mpango amesema kuwa suala la usimamizi wa Maafisa Ugani. Sambamba na jitihada za Serikali kusomesha na kuajiri maofisa hao na kuwapatia vitendea kazi, lazima kuanzia sasa kazi zao zisimamiwe ipasavyo.
“Itapaswa kila Ofisa Ugani kuwa na orodha ya wafugaji anaowahudumia, ratiba ya kuwatembelea wafugaji ili kuwashauri na kufuatilia maendeleo ya mifugo, na kupima matokeo ya huduma anazotoa. Maafisa Ugani wasikae maofisini. Hata mavazi yao yafaa yawe ya Uwandani.”
Aidha amesema kuwa kuanzisha mashamba darasa na mashamba ya mfano ya malisho katika vijiji na halmashauri za wilaya; mifano ya aina ya malisho ni pamoja na jamii ya kunde, nyasi au miti ya chakula kikavu cha mifugo. Aidha, maofisa ugani wenyewe wajitahidi kufuga kitaalamu kwa vitendo sio nadharia tu.
Eneo lingine ni uzalishaji na uchakataji wa chakula bora cha mifugo na uchimbaji wa malambo ya maji kwa ajili ya mifugo. “Naamini SIDO, Taasisi za Teknolojia na Halmashauri wanaweza kutusaidia kama wataweka nguvu zaidi katika shughuli hizi.”
Pia kunenepesha mifugo na kuendeleza malisho. Kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya ya mifugo ikiwa ni pamoja na madawa, chanjo na majosho ili kuzuia vimelea.
Hata hivyo amesema kuwa kufundisha wafugaji kuhusu uchaguzi wa madume na majike ya mbegu ili kukuza kizazi bora cha wanyama wa asili au chotara na kuweka kumbukumbu ya upandishaji.
Kuimarisha na kueneza huduma ya uhimilishaji. Kuimarisha udhibiti wa biashara ya chanjo na madawa ya mifugo ili kuhakikisha yana ubora na bei zake zinaendana na uwezo wa wafugaji wadogo; kuzuia uuzaji wa chanjo na madawa yaliyoisha muda wake; na upatikanaji wa chanjo na madawa ya mifugo katika Vijiji na maeneo ya wafugaji.
Pia kutafuta masoko ya mifugo ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo na kupanga matumizi ya ardhi kwa ajili ya mifugo na kilimo cha mazao.
Dk Mpango amesema, Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji wa biashara katika sekta ya Mifugo. Kwa mfano katika mwaka 2021/2022 imetoa unafuu wa kodi kwa lengo la kuchochea zaidi uzalishaji, uchakataji na usindikaji wa mazao ya mifugo.
“Unafuu huo ni kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya asilimia 18 kwenye matengi maalumu ya kubeba na kusafirishia maziwa na vifungashio vinavyotumiwa na wasindikaji wa maziwa kwa joto la juu yanayodumu muda mrefu.”
Kuondoa ushuru wa forodha wa asilimia 25 kwenye malighafi inayotumika katika usindikaji wa ngozi, mashine na vipuri vya kuzalisha viatu vya ngozi.
Kubadilisha tozo ya uuzaji nyama nje ya nchi kutoka Sh 150 kwa kilo ya nyama ya ng’ombe na Sh 50 kwa nyama ya mbuzi na kuwa sh 70,000 kwa kibali kwa pamoja.
Kubadilisha tozo ya asilimia 1 ya thamani ya mzigo wa nyama inayouzwa njie ya nchi na kuwa Sh 40,000 kwa kibali.
Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika, ikitanguliwa na Ethiopia, kwa kuwa na mifugo mingi. Idadi ya ng’ombe kwa mwaka 2019/20 ilifikia milioni 33.9; mbuzi milioni 24.5; kondoo milioni 8.5; na kuku milioni 87.7.
”Licha ya Tanzania kuwa nchi ya pili kwa idadi ya mifugo Barani Afrika lakini bado tija ya sekta hiyo hairidhishi kutokana na kukosekana kwa huduma bora za ugani pamoja na wananchi kuendeleza utamaduni wa ufugaji wa kienyeji ambao hauzingatii ubora”amesema Dkt.Mpango
Kiwango cha umasikini katika mikoa yenye mifugo mingi kama vile Mwanza, Simiyu, Manyara na Tabora kilikuwa zaidi ya asilimia 30, ukilinganisha na wastani wa kitaifa wa asilimia 26.4.
Miongoni mwa sababu zinazopelekea mchango mdogo wa sekta hii katika Pato la Taifa na kurudisha nyuma jitihada za kupunguza umaskini ni pamoja na kuendelea kwa utamaduni wa ufugaji wa kienyeji ambao hauzingatii ubora bali idadi kubwa ya mifugo, hali inasababisha uwezo mdogo wa kukabiliana na magonjwa ya mifugo.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekabidhi pikipiki 300 kwa wakuu wa Mikoa wakiwakilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka ili kutumika kwa kazi za maafisa Ugani katika Halmashauri 140 hapa nchini.
Makamu wa Rais ameagiza pikipiki hizo kutumika kwa malengo yaliokusudiwa ambayo ni kuwahudumia wafugaji katika maeneo yao na si vinginevyo.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema kuwa kikao hicho kinalenga kupata namna bora itayosaidia kuongeza tija, kipato na kuongeza ajira katika sekta ya mifugo nchini.
Aidha amesema kutokana na hali ya ukame hapa nchini tayari baadhi ya maeneo yamekabiliwa na upungufu wa malisho ya mifugo na hivyo kupelekea kufa kwa mifugo ambapo Jumla ya Ng’ombe 69751, mbuzi 11024, kondoo 15742 na Punda 1680 zimekufa.
Katika kukabiliana na hali hiyo Waziri Ndaki amesema tayari wamezungumza na mamlaka za mabonde ya maji ili kuruhurusu mifugo kupata maji katika maeneo ya mabonde hayo pamoja na kufanya mazungumzo na mamlaka za hifadhi mbalimbali kuruhusu mifugo kupata malisho ndani ya hifadhi ili kunusuru hali hiyo.