Mkuu wa shule ya Sekondari ya wasichana Mbinga Ifigenia Nzota kulia akitoa taarifa ya kukamilika kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa vilivyojengwa chini ya Mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19 kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kushoto,ambapo Nzota amewataka wazazi kutumia fursa ya kujengwa kwa madarasa na kuboreshwa kwa miundombinu ya sekta ya elimu kupeleka watoto ili kuwajengea misingi ya maisha yao.
……………………………………….
Na Muhidin Amri,Mbinga
WAZAZI na walezi katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,wametakiwa kutumia fursa ya uwekezaji wa miundombinu katika sekta ya elimu inayofanywa na Serikali kujenga vyumba vya kisasa vya madarasa kupeleka watoto wao kupata elimu bora.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa shule ya Sekondari ya Wasichana Mbinga(Mbinga Girls) Ifigenia Nzota,wakati wa mapokezi ya wanafunzi waliochaguliwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza katika shule hiyo na kuwaomba kuhakikisha watoto wao wanafika mapema shuleni ili kuwahi muhula mpya wa masomo.
Nzota alitumia nafasi hiyo,kuwaonesha wazazi na wanafunzi hao baadhi ya madarasa mapya yaliyojengwa na Serikali ya awamu ya sita kwa fedha za Mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19.
Alisema,Shule ya Wasichana Mbinga, imejipanga kutoa elimu yenye ubora wa hali ya juu kwa kuhakikisha wanafunzi wanasoma kwa vitendo ili kuwasaidia kufanya vizuri katika masomo yao.
Nzota, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa jitihada anazofanya ikiwamo kutafuta fedha ambazo zimetumika kujenga vyumba vipya vya madarasa na miundombinu ya elimu katika shule mbalimbali hapa nchini.
Ametoa wito kwa wazazi na walezi wilayani humo, kupeleka watoto wao kusoma mapema ili waweze kunufaika na uwekezaji wa majengo mapya uliofanywa na Serikali na walimu waweze kutekeleza mipango yao kwa wakati na mwisho wa mwaka wapate matokeo mazuri katika masomo na mitihani yao.
Amehaidi kuwa, katika muhula wa masomo wa mwaka 2022 walimu wa shule hiyo wamejipanga kutumia fursa ya ujenzi wa madarasa mapya yaliyogharimu jumla ya Sh.milioni 41 kufundisha kwa bidii ili jitihada zilizofanywa na Serikali zilete tija sio kwa wanafunzi tu bali hata kwa Serikali ambayo imedhamiria kuinua na kuboresha elimu hapa nchini.
Mkuu huyo wa shule alisema,kiujumla hali ya kitaaluma katika shule hiyo ni nzuri na wataendelea kufanya vizuri na kuwafanya watoto kuwa imara na waongeze juhudi katika masomo yao kutokana na maboresho ya kitaaluma na huduma nzuri zinazotolewa.
Aidha,amewataka wanafunzi waliopangiwa kusoma katika shule hiyo, kutumia vyema fursa ya kuwepo kwa miundombinu bora ya elimu kusoma kwa bidii na kusikiliza wanachofundishwa darasani ili waweze kutumiza ndoto zao.
Amewataka kutunza madarasa hayo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu, na kuepuka kufanya uharifu ambao unaweza kusababisha madarasa hayo kuchakaa mapema na kushindwa kufanikisha malengo ya Serikali yao.
Amewaomba wadau kutoka ndani na nje ya nchi, kujitokeza kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali kwa kuchangia ujenzi wa miundombinu ya shule kama vile ujenzi wa mabweni,maabara na vifaa ambavyo vitawezesha wanafunzi kusoma vizuri na walimu kutekeleza wajibu wao.
Baadhi ya wanafunzi walioanza kufika kwa ajili ya kuanza safari ya masomo katika shule hiyo,wameishukuru serikali kwa kutoa fedha ambazo zimetumika kuboresha miundombinu ya elimu na kujenga vyumba viwili vya madarasa.
Konsolatha Mkui wa kidato cha kwanza, ameishukuru Serikali kwa kujenga madarasa mazuri na kuhaidi kuwa,watatumia madarasa hayo kusoma kwa bidii na kupata matokeo mazuri katika masomo ambayo yaitangaza shule hiyo.
Mwanafunzi mwingine Catherine Mwakalobo alisema, madarasa hayo yatapunguza tatizo kubwa la msongamano wa wanafunzi madarasani.
Hata hivyo, ameiomba Serikali kuangalia suala la ujenzi wa mabweni na nyumba za walimu ili watoto wapate muda wa kukaa shuleni badala ya kutokea nyumbani ambako kuna changamoto nyingi.