WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema maamuzi yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kumkaribisha muwekezaji wa ujenzi wa kiwanda cha mbolea cha Itracom ni sahihi kwa maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Amesema Serikali itasimamia ujenzi wa mradi huo ili kuhakikisha azma ya Mheshimiwa Rais Samia ya kuendeleza sekta ya kilimo inafikiwa kwa sababu changamoto kubwa iliyokuwa inawakabili wakulima wengi ni upatikanaji wa mbolea ambayo inakwenda kuwa historia.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Januari 15, 2022) wakati akizungumza na uongozi na wafanyakazi wanaojenga kiwanda hicho katika eneo la Nala jijini Dodoma. “Serikali imedhamiria kuimarisha sekta ya kilimo ili Watanzania wanaoitegemea wapate mafanikio.”
Mheshimiwa ambaye leo alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wake na kwamba Serikali inataka kuona Watanzania wengi wananufaika na uwekezaji huo. Ujenzi wa kiwanda hicho umefikia asilimia 52.
“Ujenzi wa kiwanda hiki ni matokeo ya ziara ya Mheshimiwa Rais Samia nchini Burundi, lengo ni kuhakikisha tunazalisha mbolea hapa nchini badala ya kutegemea kuagiza nje kwa kiasi kikubwa. Kiwanda hiki kinatarajiwa kuzalisha tani laki 600,000 kwa mwaka,” amesema.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaagiza wataalamu wa Wizara wa Kilimo wahakikishe mbolea itakayozalishwa kiwandani hapo inakwenda sambamba na mahitaji halisi ya wakulima nchini kutokana na aina ya udongo wa maeneo husika.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ahakikishe barabara inayokwenda kiwandani hapo ikarabatiwe ili iweze kutupitika vizuri katika kipindi chote cha mwaka na kurahisisha usafirishaji wa mizigo mbalimbali ikiwemo mitambo.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Wizara ya Kilimo itatoa ushirikiano wa kutosha kwa muwekezaji huyo. Amesema mahitaji ya mbolea kwa sasa nchini ni wastani wa tani 700,000 kwa mwaka, hivyo ujenzi wa kiwanda hicho ambacho kinatarajiwa kuzalisha tani 600,000 kwa mwaka kitasaidia kuondoa na upungufu wa mbolea. Tanzania inatumia dola milioni 450 kuagiza mbolea nje.
Naye, Naibu Waziri wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema wizara yao inatambua uwekezaji mkubwa uliofanyika katika eneo hilo ambao pamoja na mambo mengine unakwenda kulisaidia Taifa katika kuokoa fedha nyingi za kigeni zinazotumika kuagiza mbolea nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde amesema mbali na kutatua tatizo la upatikanaji wa mbolea pia kiwanda hicho kinakwenda kupunguza tatizo la upatikanaji wa ajira hususan kwa vijana kwani wengi wataajiriwa.
Awali, Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Musafiri Dieudonnee alisema kiwanda hicho kitakapokamilika kinatarajiwa kuzalisha tani 600,000 za mbolea na tani 300,000 za chokaa kwa mwaka na tayari wamefikia asilimia 52 ya ujenzi wake. Amesema jumla watumishi 1,000 wameajiriwa kwa sasa na kati yao 800 ni Watanzania na 200 ni raia wa Burundi,
Naye, Mkurugenzi wa Biashara wa Itracom Fertilizer LTD, Nazaire Nduwimana alitumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini hivyo kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa usalama wa hali ya juu. “Tunaanza uzalishaji mwezi June mwaka huu,”. Kiwanda hicho kinajengwa na muwekezaji kutoka Burundi.