Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amekutana na Balozi wa Malawi nchini Mhe. Glad Chembe Munthali leo tarehe 14 Januari 2022 katika ofisi za Wizara jijini Dodoma .
Katika mazungumzo yao Mhe. Waziri Mulamula amempongeza Mhe. Munthali kwa kumaliza salama muda wake wa utumishi katika nafasi ya Balozi hapa nchini na amemtakia utumishi mwema katika majukumu mengine mapya atakayopangiwa.
“Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Malawi kwakuwa ushirikiano wetu umejikita katika kuhakikisha maendeleo ya watu na Taifa yanapatikana katika pande zote mbili za ushirikiano”.
Pia akaeleza miradi ya ushirikiano inayofanywa baina ya Tanzania na Malawi itaendelea kusimamiwa kwa karibu mpaka pale atakapoteuliwa mwakilishi mwingine kushika nafasi hiyo.
Naye Balozi Munthali alitumia nafasi hiyo kutoa shukurani zake pamoja na za Serikali ya Malawi akieleza kuwa miaka mitatu ya utumishi wake hapa nchini imekuwa ya mafanikio kufuatia ushirikiano uliotolewa na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza majukumu yake.
“Tanzania kwangu ni nyumbani, sisi ni majirani na siku zote watu wetu wamekuwa na muingiliano kupitia shughuli za kiuchumi na kijamii”.
Pia, Mhe. Munthali akampongeza Mhe. Waziri Mulamula kwa utaratibu mzuri uliowekwa na Wizara katika kuhakikisha taratibu zote za Mabalozi na Wawakilishi wa Kimataifa zinasimamiwa na kuruhusu utekelezaji wa majukumu yao.
Tanzania na Malawi zimekuwa zikishirikiana katika sekta ya ujenzi wa miundombinu, huduma za jamii, biashara na masoko.