Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nauye akizungumza mbele ya Wombolezaji waliofika kuaga miili ya wanahabari watano katika uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel (kushoto) akimpa salamu za Pole Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye (kulia) wakati wa shughuli ya kitaifa ya kuaga miili ya waandishi wa habari watano waliofariki kwenye ajali ya gari iliyotoea katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Robert Gabriel akielekea Wilaya ya Ukerewe jana Januari 11,2022.
Wa pili kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Molle,kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagina Wombolezaji wengine wakifuatilia yaliyokuwa yakijiri uwanjani hapo wakati wa shughuli ya kuaga miili ya Waandishi wa Habari watano waliofariki kwenye ajali hapo jana mkoani Simiyu.
……………………………………….

Serikali imetoa muda wa siku saba kwa waajiri wote wanaodaiwa na waandishi wa habari waliofariki katika ajali ya gari wilayani Busega kulipa stahili zao.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akitoa salaamu za Serikali wakati wa hafla ya kuwaaga na kutoa heshima za mwisho kwa waandishi watano na dereva wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa mwanza waliofarika dunia jana.

“Nimepewa salaamu hapa kuwa miongoni mwa waliolala kwenye majeneza hapa mbele yangu hawajalipwa stahiki zao; natoa siku saba kwa waajiri wote wanaodaiwa kulipa stahiki zote za marehemu na kutoa taarifa ofisi ya mkuu wa mkoa,” ameagiza Nape

Akionesha msisitizo kuhusu agizo hilo, Waziri huyo aliwataka wamiliki wa vyombo vya habari wanaodaiwa kutambua kwamba, wizara yake ndiyo imeshikilia leseni zao.

“Yawezekana kuna hali ngumu ya kiuchumi, lakini nasema stahiki zote za marehemu hawa zilipwe ndani ya siku saba. Hayo ya hali ngumu tutayazungumza huko mbeleni kwa waandishi ambao wako hai,Ila kwa hawa marehemu lazima walipwe,” ameagiza Waziri Nape

Awali, wawakilishi wa waandishi wa habari waliotoa salaam walimwomba waziri huyo kushughulikia changamoto ya waandishi kutolipwa stahiki zao huku wakifichua kuwa baadhi ya marejesho hawajalipwa kwa miaka miwili iliyopita.