Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nauye ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kuchambua matukio yote ya ajali za barabarani kwenye misafara ya viongozi nchini ambayo yanachukua maisha ya wana tasnia hiyo.
Amesema hayo wakati akitoa pole kwenye hafla ya kuaga miili ya wanahabari watano mkoani Mwanza.
“Nilipokuwa nakuja huku wakubwa wangu wamenielekeza kuwa nifuatilie hili la ajali kwenye misafara ya viongozi,kwani waathirika wamekuwa ni waandishi wa habari,lazima tujue chanzo ni nini?”,amesema.
Waziri Nape amesema baada ya kukabidhiwa taarifa ya uchunguzi mambo mengine yatafuata ikiwemo kubadilisha utaratibu mzima.
Amesema utaandaliwa utaratibu maalumu au itifaki rasmi ya namna bora ya ushiriki wa wanahabari kwenye ziara hizo.
Kauli hiyo ya Nape imejibu kilio cha Wanahabari wengi nchini kuwa mara nyingi hawapewi kipaumbele kwenye ziara hizo, ambapo mara nyingi wanapewa magari yasiyo na viwango, ambayo hayawezi kuendana na mwendo wa misafara yenyewe na kujikuta yakiachwa nyuma na pale wanapojitahidi kukimbia ili kuwahi matukuio wanaishia kupata ajali na kupoteza maisha.
************
Waziri wa Habari na Mawasiliano ya teknolojia ya Habari Nape Nnauye ni miongoni mwa waliofika kwenye uwanja wa Nyamagana kungana na Mkuu wa Mkoa Mwanza Injinia Robert Gabriel na Waombolezaji wengine kuaga miili ya Wanahabari watano waliofariki kwenye ajali jana wakiwa ziarani na Mkuu wa mkoa wa Mwanza.