Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma wakati akitoa taarifa juu ya Tanzania kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa 50 wa chama cha mabunge Jumuiya ya Madola,kanda ya Afrika (CPA) kitakachofanyika visiwani Zanzibar.
Katibu wa Bunge ambaye pia ni Katibu wa CPA Kanda ya Afrika, Stephen Kagaigai,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma
………………..
Na Debora Sanja, Bunge
Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 50 wa Chama cha Mabunge cha Jumuiya ya Madola, Kanda ya Afrika (CPA) ambapo zaidi ya wageni 400 kutoka Nchi mbalimbali wanachama wanatarajiwa kushiriki Mkutano huo.
Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Dodoma, Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai alisema Mkutano huo unatarajiwa kufanyika katika Kisiwa cha Zanzibar kuanzia tarehe 31 Agosti hadi tarehe 5 Septemba mwaka huu.
Alisema ufunguzi wa mkutano huo utafanyika tarehe 2 Septemba, 2019 ambapo mgeni Rasmi atakuwa Mhe. Dkt. Mohamed Shein, Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Zanzibar.
“Wageni mbalimbali wamealikwa ikiwemo Maspika kutoka nchi wananchama, manaibu spika, wabunge na mabalozi kutoka nchi wanachama pamoja na maspika wengine kutoka mabara na Kanda nyingine,” alisema.
Alisema hadi sasa mataifa zaidi ya 13 yameshathibitisha kushiriki huku mwitikio ukiwa ni mkubwa kutokana na Mkutano huo kufanyika Tanzania hususan katika Kisiwa cha Zanzibar.
Mhe. Ndugai alisema mkutano huo utasaidia kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania pamoja na kuingiza kipato cha fedha za kigeni na kutoa fursa kwa wanyabiashara nchini kufanya biashara zao.
“Naomba kuwashauri wafanyabiashara na Watanzania wenzangu kwa ujumla fursa hizi tunazozipata za kuaminiwa na mataifa mbalimbali, tuzichangamkie, ni fursa adhimu ambazo mataifa mengine wanazililia,” alisema.
Kwa upande wake Katibu wa Bunge ambaye pia ni Katibu wa CPA Kanda ya Afrika, Stephen Kagaigai alisema maandalizi yote yanaendelea vizuri na kwamba sekratieri ya CPA ipo tayari kuhudumia ugeni huo kwa ufanisi.
Kauli Mbiu ya Mkutano wa 50 wa CPA kwa mwaka huu ni “Bunge Mtandao kwa Ajili ys Kuwezesha Demokrasia”.