…………………………………………………………………
Na. Angela Msimbira TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Innocent Bashungwa(Mb) amesema kuwa kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha inashughulikia changamoto za wananchi kuanzia ngazi ya kijiji.
Akiongea na menejimenti ya Ofisi ya Rais TAMISEMI leo muda mchache baada ya kuapishwa katika Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma Waziri Bashungwa amesema kuwa wataalamu wanatakiwa kuangalia changamoto zilizopo kwenye vijiji ili kupata picha halisi ya matatizo yanayowakabili wananchi na kupanga mipango kimakakati ya kutatua kero hizo kwa jamii.
“Ninawataka watumishi wa Ofisi ya Rais Tamisemi kujikita zaidi kwenye matatizo yanayojitokeza zaidi kwenye vijiji na kuyachukulia kuwa ni changamoto ya nchi nzima hivyo tunahitajika kuweka mikakati ya kuzitatua na kuwezesha wananchi katika kutoa huduma bora,”amesema Waziri Bashungwa.
Amebainisha kuwa watumishi wanapaswa kujifunza kwenye ngazi za vijiji ili changamoto wanazopata wananchi ikiwemo ukosefu wa madarasa, zahanati na mengineyo zitatuliwe haraka iwezekanavyo.
Waziri Bashungwa amesema utatuzi wa changamoto hizo itasadia kutoa huduma bora kwa wananchi na kuzingatia hilo wakati wa uandaaji wa bajeti za kila mwaka kwenye wizara husika.
Vilevile Waziri Bashungwa amewataka wataalam ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanafanya tathmini na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo kwa kuangalia uhalisia wa fedha ziliziopelekwa na dhamani ya miradi inayotekelezwa hasa katika ngazi za vijiji ili kupata uhalisia wa matumizi ya fedha zinazotolewa na serikali.
Aidha, ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia kwa kumteua kushika wadhifa huo na kuahidi kuwa atatimiza wajibu wake kwa kushughulikia changamoto mbalimbali za watumishi na wananchi.
Waziri Bashungwa amesisitiza matumizi ya mifumo kwa watumishi wote wa mamlaka za Serikali za Mitaa itakayorahisha ufuatiliaji na utendaji kazi ili kupata taarifa za utekelezaji wa miradi kwa wakati.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais -TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Mhe. David Silinde amewataka watumishi kuongeza ushirikiano katika utekelezaji majukumu yao ili kutatua kero za wanachi na kutoa huduma bora kwa jamii.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais- TAMISEMI anayesghulikia Afya Dk Festo Dugange amemuahidi Waziri Bashughwa kuwa watampa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji majukumu yake.
Katibu Mkuu TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe amesema kwa ushirikiano mkubwa wa watumishi kwa sasa umefanyika ujenzi wa madarasa 15560, vituo vya afya 233 huku miradi mbalimbali ikitekelezwa.