Alisema huko nyuma utaratibu wa kupata viongozi walioandaliwa ulianza kupotea na kusababisha nchi kupata viongozi ambao hawajapikwa kiungozi, ndio maana yeye na baadhi ya wanasiasa wakongwe (makada) nchini wamepongeza uteuzi huo kwa heshima kubwa.
Mgeja alisema kuwa ni hatari kubwa kwa taifa huko mbele ya safari kunaweza kutokea ombwe kubwa la kupata viongozi makini ambao hawakujaandaliwa lakini kwa uteuzi wa hivi karibuni Rais samia ameangalia mbali.
Mwenyekiti huyo wa Tanzania Mzalendo Foundation inayojishughulisha na masuala ya haki, demokrasia na utawala bora alisema ilifika mahala hata wateule walioteuliwa waliona kuteuliwa kwao ni bahati ya mtende na kuufananisha na embe kuanguka chini ya mbuyu.
Alisema hali hiyo ilisababisha baadhi ya wateule kulewa sifa huku wakijinasibu kuteuliwa kwao ni bahati kubwa ya pekee na wengine walisifikia kudai kuokotwa jalalani, kwa vile wana uwezo mkubwa wa kielimu lakini hawakuwahi kupewa fursa ya uwaziri kwa miaka dahari.
Mgeja alishangaa kama mtu ameokotwa jalalani na kupewa uongozi kweli ni hatari kubwa sana kwa mustakabali wa uongozi wa nchi hayo ni madhara ya kuteua viongozi ambao hawajaandaliwa na baadhi yao kupatikana kutoka jalalani.
“Hoja hapa si elimu kubwa bali ni kuandaliwa kiuongozi.Kama kweli wao waliona ni sifa ya kiuongozi kuokotwa jalalani, basi ni vyema wakajisifu tena kwa kurudishwa jalalani kwenye asili yao walikotokea,”alisema Mgeja.
Akizungumzia upatikanaji wa viongozi bora walioandalika huko nyuma,alisema kwa miaka mingi viongozi wazuri au vijana wenye maono na karama za uongozi walichafuliwa sana na akaonya kuna kikundi cha baadhi ya watu wahafidhina kazi yao kubwa ni kuchafua watu wengine na kuvunja heshima zao .
Alidai kundi hilo limekuwa likijipambanua kuwa ni safi sana mithili ya malaika huku wakiwafananisha wengine ni wachafu kama mashetani lakini wanasahau kuwa katika nchi hii watu wote wana haki sawa.
Alieleza kuwa mchezo huo mchafu unaotokana na kundi au genge ambalo kazi yake kubwa ni kuwadhoofisha na kuwachafua vijana hasa wanapoona vijana wanaelekea kufanya vizuri na viongozi wazuri hapa nchini huanza kushughulikiwa mapema ili wananchi wakose imani nao na kuwachukia, tabia iliyojengeka muda mrefu na inaapaswa kupuuzwa.
“Nawashukuru na kuwapongeza Watanzania wengi, hivi sasa watu wana uwezo wa kuchambua mambo hasa yasiyothibitika kisheria na mengi hujaa tuhuma na mkatati mchafu wa kuchafuana, uelewa wa watanzania wengi hivi sasa ni ukombozi wa kupata maendeleo yanayosukumwa na viongozi bora wenye weledi,”alisema Mgeja.
Mwenyekiti huyo wa zamani wa CCM Mkoa wa Shinyanga, aliwaomba Watanzania kuendelea kushirikiana kwa nguvu zote na serikali iliyopo madarakani ili kazi ziendelee za kujiletea maendeleo na kwa pamoja tunaweza.