Taarifa kwa Vyombo vya Habari 

Siku za hivi karibuni kumekuwepo na taarifa za kupotosha ambazo  zimekusudia kuwahadaa Watanzania kupitia mitandao ya Kijamii hususan  YouTube, kwamba Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Salvatory  Mabeyo anaingilia kati sakata la Mhe. Rais na Spika. Jambo ambalo siyo la  kweli. 

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linasikitika na  linawaomba wananchi kuzipuuza taarifa zilizowekwa kwenye mtandao huo kupitia kwenye channel inayojiita NEWS 24 zenye kichwa cha habari  ‘‘KIMENUKA MKUU WA MAJESHI MABEYO ATOA AMRI NZITO KUJIUZULU  KWA NDUGAI’’ na ‘‘MKUU WA MAJESHI MABEYO AINGILIA KATI SAKATA  LA RAIS NA SPIKA’’. 

Ukweli ni kwamba, kikundi cha watu wachochezi kimetoa taarifa za  uongo na uzushi kwa kutumia sauti isiyo ya Mkuu wa Majeshi huku  wakiwaaminisha Umma kuwa ni sauti ya Jenerali Mabeyo kwamba aingilia  kati sakata la Mhe. Spika.  

1

JWTZ linawaomba Umma wa Watanzania kutoziamini taarifa hizo na  wazipuuze kwa kuwa ni taarifa za uzushi na uchochezi zinazotungwa na  kusambazwa na kikundi cha watu wasioitakia mema nchi yetu kwa maslahi  yao binafsi. 

Mkuu wa Majeshi hajatoa taarifa yoyote kuhusiana na yaliyozushwa  kwenye mitandao kwa kuwa JWTZ halijihusishi kwa njia yoyote ile na  masuala ya kisiasa na kamwe halitafanya hivyo. 

JWTZ linatoa onyo kwa wale wote wanaotumika kumchafua Mkuu wa  Majeshi, kwa lengo la kutaka kuliingiza Jeshi kwenye siasa. Kamwe watu  hao hawatafumbiwa macho na pindi watakapobainika hatua kali  zitachukuliwa dhidi yao ili liwe fundisho kwa wengine. 

Tunawaomba watanzania wote kuungana kwa kuendelea kupuuza na  kukemea vikali taarifa hizo ambazo hazilitakii mema Taifa letu. 

Nitumie fursa hii kuwahakikishia Watanzania wote kwamba JWTZ lipo  imara, linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa mujibu  wa Katiba kulinda na kuimarisha mipaka ya nchi yetu. Aidha, JWTZ  linatekeleza majukumu yake ya msingi na lina mipaka yake kama  yalivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Daima JWTZ litamlinda na kumtii Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu.