Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Batilda Salha Burian (wa tatu kutoka kulia-walioketi mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Mameneja wa Mamlaka ya Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA) kutoka wilya zote 7 za Mkoa huo, wa kwanza kulia (walioketi) ni Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tabora Mhandisi Hatari Kapufi. Picha na Lucas Raphael,
…………………………………………………….
Na Lucas Raphael,Tabora
WAKURUGENZI wa halmashauri Mkoani Tabora wametakiwa kusimamia ipasavyo utendaji wa Vyombo vya Watoa Huduma za Maji kwa wananchi waishio vijijini (CBWSO’s) ili kuongeza ufanisi.
Rai hiyo imetolewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian alipokuwa akiongea na wadau wa maji katika hafla ya utiaji saini mikataba ya utekelezaji miradi ya maji katika wilaya zote za Mkoa huo.
Alisema kuwa vyombo hivyo vimepewa dhamana ya kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inawafikia wananchi waishio vijijini ili kuwapunguzia adha ya ukosefu wa huduma hiyo.
Alisisitiza kuwa kama vyombo hivyo vitasimamiwa ipasavyo na kuwezeshwa na mamlaka husika (Wizara ya Maji na Wakala wa Usambazaji Maji Vijijini) huduma hiyo itafikia wananchi walio wengi na kwa wakati.
Dkt Batilda alifafanua kuwa wajumbe wa Kamati zinazosimamia vyombo hivyo wengi wao ni Watendaji na Waheshimiwa madiwani ambao wako chini ya halmashauri hivyo Wakurugezi wanapaswa kusimamia na kufuatilia utendaji wake.
Aidha aliwataka kushirikiana na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama ili kuhakikisha vyanzo vya maji, mali, vifaa na miundombinu ya maji vinalindwa ili kufikia matokeo yaliyokusudiwa.
‘CBWSO’s zimeundwa ili kufanikisha utekelezaji ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 ambayo inaelekeza kuwa ifikapo mwaka 2025 huduma ya maji vijijini iwe imefikia asilimia 85 na mjini asilimia 95’, alisema.
Balozi Batilda aliwataka Wataalamu wa Wakala wa Usambazaji Maji vijijini (RUWASA) kufuatilia kwa karibu zaidi utendaji wa vyombo hivyo ikiwemo kutatua changamoto za kiutendaji wanazokabiliana nazo.
Alibainisha takwimu za hali ya upatikanaji maji katika Mkoa huo kwa maeneo ya mjini kuwa ni wastani wa asilimia 75 ambapo kwa manispaa ya Tabora ni asilimia 92, Nzega Mjini (96.5), Igunga Mjini (98), Uyui Mjini-Isikizya (92), Urambo Mjini (32) na Sikonge Mjini (39).
Aidha hali ya upatikanaji maji kwa maeneo ya vijijini alisema ni wastani wa asilimia 62.4 ambapo takwimu zinaonesha Nzega ni asilimia 82.5, Uyui (65.6), Igunga (77.6), Sikonge (63.4), Urambo (55) na Kaliua (30).
Alifafanua kuwa maeneo yote yanayosimamiwa na Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira ambazo ni Igunga, Nzega, Isikizya na Tabora upatikanaji huduma ya maji safi umeboreshwa kutokana na kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji ya ziwa Viktoria ambao umegharimu kiasi cha sh bil 640 na kupita katika vijiji 102.