Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lusius Raphael Mwenda (katikati) akiitaka Kamati ya Mawasiliano ya Wizara hiyo kuhakikisha wananchi wanapata Habari kwa wakati, kulia ni Mkuu wa Hazina Ndogo Mkoa wa Morogoro, Onesmo Ilomi na kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara hiyo, Bw. Benny Mwaipaja, mjini Morogoro.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja, akiahidi kuisimamia vema Kamati ya Mawasiliano ya Wizara hiyo, wakati wa Kikao kazi, mjini Morogoro.
Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Bw. Lusius Raphael Mwenda (katikati), Mkuu wa Hazina Ndogo Mkoa wa Morogoro, Onesmo Ilomi (kulia) na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara hiyo, Bw. Benny Mwaipaja, wakifuatilia mafunzo ya masuala ya Mawasiliano, mjini Morogoro.
Mtoa mada wakati wa kikao kazi cha Kamati ya Mawasiliano ya Wizara ya Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo cha Muslim Morogoro, Bw. Hassan Mohamed Issa, akitoa mada wakati wa Kamati hiyo, mjini Morogoro.
Kikao Kazi cha Kamati ya Mawasiliano ya Wizara ya Fedha na Mipango kikiendelea mjini Morogoro.
Mjumbe wa Kamati ya Mawasiliano wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Fundi Makama, akizungumza wakati wa Kikao kazi cha Kamati hiyo, mjini Morogoro.
Maafisa Mawasiliano wa Wizara ya Fedha na Mipango wakifuatilia mada wakati wa Kikao Kazi cha Kamati ya Mawasiliano ya Wizara hiyo, mjini Morogoro.
Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lusius Raphael Mwenda (kushoto) na Mkuu wa Hazina Ndogo Mkoa wa Morogoro, Onesmo Ilomi, wakifurahia jambo wakati wa Kikao Kazi cha Kamati ya Mawasiliano ya Wizara hiyo, mjini Morogoro.
Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lusius Raphael Mwenda (katikati), Mkuu wa Hazina Ndogo Mkoa wa Morogoro, Onesmo Ilomi na (wa pili kulia) na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara hiyo, Bw. Benny Mwaipaja (wa pili kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Mawasiliano ya Wizara hiyo, mjini Morogoro.
(Picha na Peter Haule, WFM, Morogoro)
******************************
Na. Peter Haule na Saidina Msangi, WFM, Morogoro
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu ameitaka kamati ya Mawasiliano ya Wizara hiyo kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kwa umma kwa kuwa ni haki ya wananchi kupata taarifa kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
Agizo hilo limetolewa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Rasilimali watu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lusius Raphael Mwenda, wakati wa uzinduzi rasmi wa Kamati ya Mawasiliano ya Wizara ya Fedha na Mipango iliyowakutanisha wajumbe kutoka kwenye Idara na Vitengo vya Wizara hiyo wakati wa kikao kazi, mjini Morogoro.
Alisema Kamati ya Mawasiliano ni kiungo muhimu cha masuala ya mawasiliano kati ya Idara/Vitengo na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, ambacho ndicho kimepewa majukumu ya kuwasiliana na wadau wetu muhimu wanaotarajia au wanaotegemea kupata taarifa kutoka kwenye kamati kwa ajili ya matumizi yao mbalimbali yakiwemo ya kiutafiti.
‘’ Ni matumaini yangu kwamba kila mmoja wenu atawajibika kikamilifu kukusanya taarifa zinazohitajika kutoka kwenye idara husika kama mtakavyo jadiliana na kufikia muafaka, ili kuimarisha masuala ya mawasiliano kimkakati zaidi na wadau wetu waweze kunufaika na uwepo wa kamati hii”, alieleza Dkt. Kazungu.
Alisema kuwa miongoni mwa kazi ya kamati hiyo ni pamoja na kuratibu taarifa zinazohusu Kitengo au Idara, kukusanya na kuandaa taarifa zinazopaswa kutolewa kwa Umma na kuziwasilisha Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, kuandaa taarifa za utekelezaji na kuandaa taarifa za zitakazotumika katika majarida, vipeperushi na mabango.
Aidha pamoja na majukumu waliyopewa kamati hiyo, ametoa angalizo la kufuata utaratibu wa kutoa taarifa kwa kuwa kuna watu maalumu waliopewa kibali cha kufanya kazi hiyo kwenye Wizara, Idara na Taasisi za Serikali ambapo kwa upande wa Wizara waliopewa jukumu hilo ni Katibu Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini ambaye pia ni Msemaji wa Wizara hiyo.
Vile vile Dkt.Kazungu amempongeza, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bw. Benny Mwaipaja kwa kuandaa Kikao kazi kinachoendana na mafunzo ya kuwajengea uwezo wana Kamati ya Mawasiliano ya Wizara hiyo kuhusu masuala ya Mawasiliano ya Kimkakati yatakayosaidia kufanikisha mawasiliano yenye tija kwa wadau wetu wa ndani na nje.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara hiyo, Bw. Benny Mwaipaja aliahidi kusimamia kamati vizuri na kutoa mrejesho kwa ngazi husika, pia alieleza kuwa wajibu wa kamati ni kuisogeza Wizara karibu ya wananchi na washirika wa maendeleo ili wajivunie uwepo wa Wizara kwa wao kupata habari za kweli zitakazotolewa kwa wakati ili wazitumie kwa malengo yaliyokusudiwa.
Alisema kuwa katika kikao kazi hicho wanakamati watapitia na kuchambua utekelezaji wa Mkakati wa Mawasiliano wa Wizara ambao tayari umeridhiwa na kusainiwa na Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali kwa ajili ya utekelezaji.
Alisema kuwa Mkakati huo umeainisha masuala ya msingi ya namna ya kuwasiliana na umma, aina ya ujumbe unaotarajiwa kutolewa, njia za kutumia kufikisha ujumbe husika, pamoja na tathmini na ufuatiliaji wa mawasiliano ili kuhakikisha kuwa ujumbe unawafikia wadau pamoja na kulinda taswira ya Wizara.