Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACF) Puyo Nzalayaimisi akemea vikali utupwaji wa watoto vyooni, wakati akiwasilisha taarifa ya kufunga mwaka 2021.
…………………………………………………………….
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatoa taarifa kwa umma juu ya utekelezaji wa majukumu ya Jeshi, kuanzia mwezi Januari hadi Disemba, 2021 limekabiliana na majanga ikiwemo ya moto, maokozi na ajali za barabarani pamoja na mafuriko. Jeshi linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria namba 14 ya mwaka 2007 THE FIRE AND RESUE FORCE ACT pamoja na kanuni zake. Dhima ya Jeshi ni kuokoa maisha na mali ili kukuza usalama kwa umma, kupokea miito yote ya dharura, kutoa msaada ndani ya jamii kwa ufanisi na kwa mujibu wa muongozo wa Sera ya Taifa na viwango vya kimataifa.
Katika kipindi cha Januari mpaka Disemba, 2021 Jeshi limekabiliana na matukio ya moto 1803 ambayo yamesababisha vifo vya watu 32, na majeruhi 145.
Jeshi limefanya maokozi katika ajali za barabarani, mafuriko, kwenye migodi, mashimo ya vyoo, visima, mito, baharini pamoja na maeneo mengine. Jumla ya maokozi 694 yalifanyika, matukio hayo ya maokozi yalisababisha vifo 388 na majeruhi 763.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limebaini majanga mengi ya moto yanatokana na uzembe, hujuma na hitilafu za umeme kwa watu kujiunganishia umeme kiholela. Tunaendelea kufanya uchunguzi wa majanga ya moto kwenye maeneo yote ili kubaini vyanzo zaidi vya majanga hayo.
Jeshi linaendelea kutoa elimu katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili kuwajengea uwezo wananchi kupata uelewa wa majnga mbalimbali na namna ya kujikinga pale yanapotokea. Aidha kwa kipindi kuanzia Januari hadi Disemba, 2021 tumetoa elimu katika maeneo 2,474 na wamenufaika watu 197,183 wamefikiwa kupata elimu hii moja kwa moja tukiacha waliopata elimu kupitia vyombo vya Habari na mitandao ya kijamii.
Utoaji wa elimu unaenda sambamba na kufanya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya majanga ya moto. Ukaguzi huu ufanyika katika majengo binafsi, kibiashara, pamoja na majengo ya Serikali. Katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Disemba, 2021 tumefanya ukaguzi katika jumla ya majengo 19,202
Serikali inaendelea kuliwezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kulipatia vifaa vya kisasa vya kuzimia moto na maokozi, magari mawili ya kisasa yako katika hatua za mwisho za matengenezo pamoja na boti tatu za maokozi.
Serikali katika kulijengea Jeshi uwezo kiutendaji imetoa kibali cha ajira kwa askari 250 taratibu za usaili zimekamilika iwapo watafuzu mafunzo ya kijeshi wataajiriwa. Pia katika kuwapa motisha Maafisa na Askari, Serikali imewapandisha vyeo Maafia na Askari 925 ambao wamepanda vyeo kwa ngazi mbalimbali.
Mkakati wa Jeshi kwa mwaka 2022 ni kufanya ukaguzi na kutoa elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto ili kuendelea kuyapunguza majanga hayo.
Nawasihi wananchi ni vyema wazingatia na kufuatilia elimu zitolewazo na Jeshi lakini niwaombe Waandishi wa habari wote nchini tushirikiane kwa pamoja kuweza kuwa mabalozi wazuri katika kuuelimisha umma juu ya kinga na tahadhari dhidi ya Majanga.
Mwisho niwakumbushe wananchi wote kuhakikisha wanapitisha ramani zao za majengo katika Ofisi za makamada wa Mikoa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili waweze kupata elimu zaidi juu ya ujenzi ambao utazingatia kinga na tahadhari dhidi ya majanga.
Tushirikiane kupunguza majanga kwa kupiga namba ya dharura 114 wakati wote wa majanga ya moto na mahitaji ya huduma za Uokoaji.