………………………………………………………
Adeladius Makwega,Dodoma.
Kwa hakika tulijulisha kupitia taarifa ya habari ya Redio Tanzania Dar es Salaam ya saa mbili usiku kuwa mwaka 1990 wanafunzi 2000 na ushehe wamefaulu kidato cha kwanza na kujiunga na shule kadhaa za sekondari Mkoani Dar es Salaam.
Nilimjulisha rafiki yangu aliyekuwa akisoma shule ya Msingi ya Sokoine Mtoni Wilayani Temeke anayefahamika kama Fredy Mwambene juu ya kutolewa kwa matokeo hayo na tulifunga safari hadi Shule ya Uhuru Mchanganyiko kutazama kama majina yetu yalikuwepo katika kitabu hicho.
Kwa kuwa tulikuwa tunatokea Mbagala tulifika Shule ya Uhuru Mchanganyiko na kukutana na wanafunzi wengi wakitazama majina yao katika kitabu hicho kila mmoja alikaa foleni na tulipofika katika kitabu tuliangalia majina yetu katika kila shule za sekondari za Dar es Salaam na mimi na rafiki yangu Mwambene kutambua kuwa tumepangiwa Tambaza Sekondari.
Muda huo huo tulifunga safari hadi Tambaza Sekondari na kuchukua fomu zetu za kujiunga, tulitembea kwa mguu kutoka shule ya Msingi ya Uhuru Mchanganyiko hadi Muhimbili na kufika hapo Tambaza Sekondari, kila mmoja alipatiwa fomu yake ya kujiunga na shule hiyo ambayo ilikuwa na jina lake.
Shule hii ilikuwa katika mazingira ya utulivu sana jirani na barabara ya Umoja wa Mataifa, ambayo ilikuwa ikipita magari ya kibalozi na magari binafsi machache sana lakini yakiwa na kasi kubwa na hakukuwa na Chai Maharagwe au Daladala zozote hata moja zilizokuwa zikipita jirani na shule hii. Daladala zote zilikuwa zinaishia nje ya geti la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tu. Nilibaini kuwa barabara ya Umoja wa Mataifa ilikuwa ni njia pekee ambayo daladala zilikuwa zinatembea umbali mfupi sana usiozidi kilomita moja nadhani hiyo ni barabara ya pekee nchini Tanzania kwa wakati huo.
Daladala /Chai Maharagwe hizo wakati huo umbali zilizokuwa zikitembea katika Barabara hii ni kutoka Fire hadi kuingilia mbele ya shule ya Azania tu, jirani za Ofisi za Mabasi ya Super Star na kupitia jirani na Posta ya Muhimbili na Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili na kufika Muhimbili Hospitali.
Hali hiyo ilikuwa tofauti na kule Shule ya Msingi Mnazi Mmoja iliyozungukwa na fujo na makelele ya magari, Shule ya Msingi Mbagala au Shule ya Msingi Mtoni Kijichi ambapo kulikokuwa na milio ya ndege tu, huko Mtoni Kijichi, mwanakwetu hakukuwa na magari yoyote kwa wakati huo labda kwa nadra sana gari kwenda kubeba embe dodo au mkaa uliokuwa ukichomwa na Wazaramo, Wandengereko au Wamakonde Maraba ambao walikuwa wakaazi wa asili wa Mtoni Kijichi hawa ni nduguze Kitwana Kondo (K.K).
Maelekezo ya shule hii ya Tambaza katika fomu ya kujiunga yalitutaka kushona shati jeupe la mikono mifupi, Kaptula ya Kitambaa cha Polista ya Kijivu, Viatu Vyeusi na Soksi Nyeusi. Huku mwanafunzi akitakiwa kulipa ada ya shilingi 2000/- ambapo 1000/- kwa muhula. Kweli niliandaliwa vifaa hivyo na shangazi yangu anayefahamika kama Honesta Makwega ambaye alikuwa Mkaguzi wa Shule za Msingi katika Wilaya ya Ilala
Nakumbuka nilipatiwa na shangazi yangu huyo viatu vya mkuki moyoni ambavyo vilikuwa vina manyoya manyoya, huku kukiwa na eneo dogo la kupiga kiwi pale zinapofungwa kamba tu, viatu hivyo vilikuwa havitumii kiwi nyingi na vilipunguza gharama sana ya kupiga kiwi kwa mafundi viatu wa Kichaga ambao wakati huo walikuwa wapiga kiwi maarufu Mkoani Dar es Salaam.
Kidato cha kwanza, tulifungua shule wiki moja kabla ya madarasa ya juu. Kweli tulifika shuleni hapo mapema baada ya kupanda mabasi kadhaa kutokea Mbagala, Temeke Shule ya Uhuru na Uhuru hadi Muhimbili getini, tulishuka na kuambaamba na Barabara ya Maliki, hapo tulikutana na Mtaa wa Mindu. Makutano ya Barabara ya Maliki na Mtaa wa Mindu, kwa mkono wa kulia kulikuwa na vibanda vya biashara kadhaa, nakumbuka kibanda kimoja wapo kilikuwa na bango la jamaa mmoja ambaye alikuwa mpishi wa pilau ambaye alifahamika kama Ali Mapilau baadae hata kwenye mahafalii ya Tambaza alikuwa akija kupika pilau hilo. Tulitembea kidogo kando kando ya makaburi ya Tambaza na kutokea Barabara ya Umoja wa Mataifa, tukakata kushoto hadi Tambaza Sekondari.
Tulisimama mstarini na kukaribishwa na Mwalimu Mkuu aliyefahamika kama Julius Mushi alikuwa mrefu, mwembamba na mweupe sana, huku akipenda kuchomekea vizuri akiwa anapenda kuvalia mashati ya mikono mifupi.
“Kwanza nawapongeza sana kwa kuchaguliwa kujiunga na shule ya Tambaza, nyinyi ni miongoni mwa wanafunzi wachache wa Kitanzania waliopata nafasi ya kujiunga na shule chache za sekondari hapa nchini, tunatarajia mkiwa hapa Tambaza mtakuwa mfano wa kuigwa na mtafanya vizuri katika masomo yenu na kuendelea mbele na mbele zaidi, wengi wenu mmefanya vizuri katika mtihani wenu wa darasa la saba huku mkifaulu vizuri katika somo la Hisabati na masomo mengineyo, kama fomu za TSM 9 zinavyoonesha, sasa mkiwa hapa, tunataka tuone huo ufaulu wenu katika masomo yenu ya sekondari. Karibuni sana Tambaza, Jina la Tambaza ni jina la waasisi walioutafuta uhuru wa nchi hii, huku wengine wakilipa maana mbalimbali kama vile Tazama Mbali Zaidi.” Aliongea Mkuu huyu wa shule kwa lafudhi ya Kichaga huku wanafunzi wote wa kidato cha kwanza tukipiga makofi kwakwakwa….
Alipomaliza alikuja mwalimu wa taaluma wa shule hii, alisema kuwa majina yetu tayari yamepangwa katika makundi mawili, kundi la kwanza na kundi la pili. Kundi la kwanza wanakuwa na nembo nyekundu katika mfuko wa shati na kundi la pili wanakuwa na nembo ya kijani.
“Madarasa hayo ya mikondo yatakuwa na herufi R 1 &R2, M1&M2,N1&N2,T1&T2,Z1&Z2 na U1&U2 huku kila darasa litakuwa na wanafunzi 40, jumla mtakuwa wanafunzi 480. Kundi la kwanza litaingia asubuhi wiki ijayo na mtapatiwa chai na kipande cha mkate kila siku mkiingia asubuhi na kundi la pili litaingia mchana na mtapatiwa chakula cha mchana kila siku mkiingia mchana. Utaratibu utakuwa wa mzunguko asubuhi, mchana, asubuhi mchana hadi mwaka ukiisha ” Alizungumza mwalimu wa taaluma shuleni Tambaza ambaye na yeye pia alikuwa Mchaga, siku hiyo hatukuambiwa lolote suala la kulipa ada hiyo wala malipo yoyote yale. Kumbuka 1000/ ile aliyonipa Mwalimu Honesta Makwega niliificha wala sikulipa karo wala kudaiwa hadi naondoka Tambaza sekondari mwaka1993
Tulipoingia darasani tulikutana na madawati mazuri ambayo kila dawati tuliketi wanafunzi wawili wawili na kila mmoja alipata pa kukaa huku dawati hilo liliweza kuwapa nafasi watu hata wanne. Tulipokaa tu tulitazama ubaoni tulikaribishwa na maandishi ya kutisha ambayo yalikuwa yakitoa vitisho vizito kwa wanafunzi sie wageni.
“Nyinyi kidato cha kwanza ni njuka tu, ole wenu mfute haya maandishi tutapambana na nyinyi, tukikukuta na form one unashangaashangaa tutakupigisha simu chooni.” Ubao huo ulichorwa picha za kutisha zenye mafuvu ya watu, michoro ya kenge, vinyonga, n’ge , tandu na nyoka na maneno mengi na michoro kadhaa ya kutisha ambayomilichorwa kwa kutumia chaki za rangi mbalimbali. Kichwani kwangu ilikuja picha kuwa sasa hapa sio pahala salama, maana yake ndundi muda wowote ule.
Tukiwa mle darasani kilikuja kikundi cha wanafunzi ambao nadhani walikuwa wa kidato cha pili,walikuwa wamevaa sare za shule huku wakiwa hawajachomekea, wachafu, wengine wamevaa mabuti mabuti, wengine wapo pekupeku, wengine vifua wazi, walikuja wakifoka, binafsi nilijiuliza maswali mengi bila ya kupata majibu. Vijana hawa waliingia huku wakiwa wamevaa kaptula za shule hii ambapo zinaonekana kuwa zote zilifumuliwa pindo nyuzi zikining’inia mithili ya kitambaa kinachofumwa. Jamaa waliingia na doo yenye kinyesi cha ng’ombe wakaijaza maji kuikoroga huku tukiona na kuanza kutumwagia bila ya huruma tukiwa tumevalia sare zetu safi.
Duu hali ilikuwa ilikuwa hatari huku kila mwanafunzi wa kidato cha kwanza akitafuta njia ya kupita mlangoni kukimbia nje nao mlango ukiwa mdogo.
Gafla waliingia darasani kundi lingine ya vijana hao na kuanza vurugu kwa mbele, huku tukipigwa masingi tukiambiwa kuwa sie ni mabishoo tu.Tambaza siyo shule ya mabisho ni shule ya magangwe. Kwa mkono wangu wa kulia alikuwa rafiki yangu mmoja anayefahamika kama Ibrahimu Liguo nilipangiwa naye dawati moja alikuwa akiishi Urafiki kabila lake alikuwa Mkamba au Mdigo. Liguo hakuwa na mwili mkubwa alikuwa mwembamba sana kama mimi, kwa hiyo tulipata msukosuko mkubwa kama asemavyo Shabani Robert kuwa mzizimo wa baridi mara zote humpata kondoo mwenye manyoya haba.
Katika madawati ya mbele alikuwepo jamaa mmoja aliyekuwa mrefu sana na ana mwili mkubwa akifahamika kama Wille John (sasa ni mhandisi), huku akiwa mwoga sana. Pia alikuwepo mwanafunzi mwingine anayefahamika kama Atanasi Luizzi (sasa ni mfanyabiashara na kada wa CCM), kidato cha pili walipofika hapo walimsumbua Wille John hakujibu mapigo, walipofika kwa Atanasi Luizzi huku akiwa amelowesha maji walipomgusa tu ndugu huyu alimpiga mtu mmoja kichwa akaanguka chini, Atanasi Luizzi alimshika jamaa mwingine ngumi hadi chini. mwingine tena chini, mwingine teke chini. Kweli mwenzetu alipoonesha ushujaa huo na siye tuliongeza nguvu ya kupambana na jamaa hawa, mwanakwetu jamaa wote wakakimbia katika darasa letu la kidato cha kwanza R1.
Atanasi Luizz alikuwa na mwili uliojengeka vizuri na kifua kipana na aliwapiga vilivyo wanafunzi wale wote na kukimbia na hawakurudi tena darasani kwetu kwa hiyo R1 tulikuwa magangwe wa Tambaza, tukawa tunatembea kwa makundi makundi katika maisha yetu yote ya kidato cha kwanza. Tulisoma kwa amani na utulivu vizuri tangu siku hiyo. Tukiwauliza waliosoma na Atanasi Luizzi shule ya msingi wakisema kuwa Atanasi alikuwa anacheza ngumi na kung fuu, hivyo aliwawezi vizuri jamaa hawa wahuni wa Tambaza. Naambiwa Atanasi Luizzi yupo Mikocheni, huyu alikuwa mtoto wa kishua tangu tukiwa shule, naamini nikipata nauli ya kwenda Dar es Salaam nitamtafuta Atanasi Luizzi nimuulize hadi sasa anaweza kupambana na wahuni kama alivyofanya wakati ule kwa wahuni wa Tambaza?
0717649257\