************************
*Asisitiza utoaji huduma bora kwa wagonjwa
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Samia Suluhu Hassan ameweka historia kwenye sekta ya afya akitoa zaidi ya sh. bilioni 495 nchi nzima ili zitumike kuboresha huduma za afya kwa Watanzania, kuboresha miundombinu, kununua vifaa tiba, dawa.
Uwekezaji huo haujawahi kufanywa na kiongozi yeyote katika awamu zote zilizopita nchini.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Godwin Mollel aliyasema hayo jana akiwa kwenye ziara ya siku moja kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo ni utaratibu wa kawaida ili kuwakumbusha viongozi na watumishi wajibu walionao kwa wagonjwa na kutoa maelekezo ili kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya afya kupitia huduma wanazotoa.
Pia Dkt. Mollel alifanya kikao cha ndani na timu za usimamizi wa hospitali na kujadiliana pamoja namna ya kuboresha huduma kwa mteja ili kuondoa malalamiko yanayotolewa mara kwa mara.
Alisema uwekezaji uliofanywa na Rais Samia katika sekta hiyo, hautakuwa na maana kama huduma wanazozitoa hazina mapokeo mazuri kwa wagonjwa.
“Tuhakikishe makosa yaliyotokea mwaka 2022 yasitokee tena mwaka huu ili uwekezaji aliofanya Rais Samia katika sekta hii uwe na manufaa kwa Watanzania.
“Fedha zilizoletwa na Rais Samia katika hospitali hii sh. bilioni 4.9, zilete matokeo katika huduma za afya, kununua vifaa tiba na kuboresha miundombinu,” alisema.
Alisema makusanyo ya hospitali hiyo kwa mwezi ni sh. milioni 350 hivyo wakiweza kuboresha huduma kwa wateja na kujipanga zaidi wanaweza kukusanya zaidi.
“Mkiboresha huduma, makusanyo yataongezeka, mtaweza kujiendesha wenyewe ili kuipunguzia mzigo serikali kuu ya kuleta fedha katika hospitali hii.
“Hospitali binafsi zilizopo ngazi ya Mkoa kama hii, zinalipwa bima saw ana hospitali yenu lakini wao wanalipa mishahara ya watumishi na kununua vifaa tiba.
“Katika hospitali ya serikali kama hii, serikali inawanunulia vifaa tib ana kulipa mishahara, lazima tuangalie, katika sh. milioni 350 mnayozalisha kila mwezi, tunazitumiaje ili kuipunguzia serikali mzigo ili fedha zinazoletwa na serikali kuu zielekezwe katika maeneo mengine,” alisema.
Alitolea mfano Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) akisema Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Profesa Mohamed Janabi anafanya kazi nzuri sana.
Alisema kila mwaka mapato ya taasisi hiyo yanapanda na kuvuka lengo kutokana na ubora wa huduma wanazotoa hivyo hospitali nyingine za serikali zijifunze kwao.
BIMA KWA WOTE
Dkt. Mollel alisema Rais Samia ametenga sh. bilioni 148.77 kwa ajili ya Bima ya Afya kwa wasiojiweza hivyo mpango wa bima kwa wote ukianza, wananchi wataamua wenyewe sehemu ya kupatiwa huduma ya matibabu.
“Tusipoboresha huduma katika hospitali za serikali, tutakosa wagonjwa wa kuwahudumia, watakwenda hospitali binafsi wakati hospitali za serikali ndizo zinazopaswa kutoa huduma bora za matibabu.
“Ndio maana wagonjwa wanapokwenda hospitali binafsi, wakizidiwa wanahamishiwa hospitali za serikali ambazo ndizo zenye wataalam na uwezo wa kutosha kuliko hospitali binafsi.
“Naomba tujipange ili tuboreshe huduma kwa wateja ili wananchi waendelee kuja hospitali za serikali na akienda hospitali binafsi awe ametaka mwenyewe lakini sio kwa kukosa huduma ambayo aliitaka lakini hajaipata,” alisema.
MGANGA MFAWIDHI
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Joseph Kimaro, alimshukuru Rais Samia kwa fedha alizotoa sh. bilioni 4.9 ambazo zitutumika kuboresha huduma katika hospitali hiyo.
Alisema pia fedha hizo zitafanya ukarabati mkubwa wa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), kununua vifaa tiba vya bilioni 1.3 kwa ajili ya ICU, kununua CT Scan yenye uwezo mzuri ili kupuguza shida za wananchi kwenda kupata huduma katika hospitali nyingine, kununua mashine nyingine ya x-ray ya kisasa zaidi.
Vifaa vyote vipo kwenye hatua tofauti za manunuzi, baadhi wamesaini mikataba, wanasubili utekelezaji. Hadi Aprili, 2022, hospitali hiyo itakuwa na mabadiliko makubwa.
Dkt. Mollel amemaliza ziara katika Hospitali za Rufaa mkoani humo ambapo leo ataendelea na ziara hiyo katika Hospitali za Taifa.