Na Abby Nkungu, Ikungi
WAKURUGENZI wa halmashauri mkoani Singida wametakiwa kujenga utamaduni wa kutenga bajeti kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa vyumba vya madarasa kila mwaka ili kuhakikisha wanafunzi wote ofaulu kwenda sekondari na wanaoandikishwa darasa la kwanza wanajiunga bila kuathiriwa na kikwazo cha kukosa nafasi.
Agizo hilo lilitolewa katika kijiji cha Issuna wilayani Ikungi na Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk .Binilith Mahenge wakati wa hafla ya kumkabidhi madarasa 664 yenye thamani ya Sh bilioni 13.4 yaliyojengwa kwa fedha za mradi wa Maendeleo ya Taifa.
“Kwa niaba yenu nyote wana-Singida, kwa heshima kubwa sana nimpongeze Mheshimiwa Rais. Hapa Singida mwaka huu tumefaulisha watoto 28,075 lakini uwezo wetu ni kuchukua wanafunzi 16,520 tu.
Sasa kama tusingepata msaada huu wa kujengewa madarasa 330 ya sekondari, ebu tujiulize hiyo patashika ya kujenga madarasa hayo kwa nguvu zetu ingekuwaje?” alihoji Dk Mahenge.
Alisema kuwa kutokana na ukweli kwamba kila mwaka idadi ya wanafunzi wanaofaulu kwenda sekondari na wanaoandikishwa darasa la kwanza inaongezeka, kuna haja kubwa ya kila halmashauri kuanza kutenga bajeti ya ujenzi wa madarasa mapya kila mwaka ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa huyo, madarasa yaliyojengwa kwa mkoa mzima kutokana na fedha hizo ni 664, madarasa ya shule za Sekondari ni 330, Shule shikizi 332 na mabweni mawili.
Aidha, Dk Mahenge alimshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha hizo na kusema kuwa licha ya fedha hizo kusaidia sekta ya elimu, pia zimesaidia kutoa ajira kwa vijana, kunufaisha wafanyabiashara na makundi mengine katika jamii kwa njia mbalimbali.
Alisisitiza umuhimu wa kila mtoto aliyeandikishwa au mwanafunzi aliyechaguliwa kujiunga na sekondari kufanya hivyo bila kukosa kwa kuwa hivi sasa hakuna tena kisingizio huku akihimiza Serikali za vijiji na mitaa kuhakikisha wanalisimamia jambo hilo kwa ukaribu zaidi.
Awali, Katibu Tawala wa mkoa, Dorothy Mwaluko akieleza taswira ya ujenzi wa madarasa hayo katikahalmashauri zote saba, alisema Singida Manispaa wamejenga madarasa 42 kwa Sh milioni 840 na Halmashauri ya wilaya ya Singida madarasa 68 kwa Sh bilioni 1.42 tu.
Alieleza kuwa Manyoni wamejenga madarasa 122 kwa Sh bilioni 2.5, Ikungi miundombinu 132 kwa Sh bilioni 2.64, Iramba madarasa 61 kwa Sh bilioni 1.22, Mkalama madarasa 83 kwa Sh bilioni 1.26 wakati Itigi wamejenga miundombinu 176 kwa Sh bilioni 3. 52 tu.
Baadhi ya wananchi wamemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha hizo za ujenzi wa madarasa kwa shule za msingi na sekondari ambapo wamesema zimesaidia kupunguza kero ya kudaiwa michango mbalimbali hali itakayowapa wasaa wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo bila bughudha.