*****************
Na WAMJW- Brazzaville
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amelipongeza Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo kwa juhudi inazofanya kwa pamoja katika kudhibiti ugonjwa wa Ebola.
Waziri Ummy amesema hayo leo wakati akiwasilisha taarifa ya mkakati wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola katika mkutano wa 69 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaojumuisha Mawaziri wa Afya kutoka nchi mbalimbali za Afrika unaoendelea jijini Brazzaville nchini Jamhuri ya Kongo.
Aidha, Waziri Ummy amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom kwa kutangaza Ebola kuwa janga la Kimataifa, na kuongeza kuwa Tanzania imefaidika na msaada wa WHO ambao umeiwezesha nchi kujenga uwezo wa utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo iwapo utaingia nchini.
Waziri Ummy amesema kumekua na uboreshaji wa mpango mkakati wa Ebola uliofanyika Mwezi Machi Mwaka 2019 ambao umelenga kuimarisha ufuatiliaji wa mgonjwa maeneo ya mipakani, kujenga uwezo wa watumishi wa afya kumtambua mgonjwa na kutoa matibabu, kununua vifaa vya kujikinga (PPE) na uratibu huu wa kukabiliana na Ebola umeshirikisha sekta mbalimbali zaidi ya Afya.
Pamoja na hayo, Waziri Ummy ametaja maeneo ambayo WHO isaidie ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza mpango mkakati wa kukabiliana na Ebola, kuimarisha ufuatiliaji katika ngazi ya jamii na kufanya mazoezi zaidi ya kupima utayari wa nchi.
Pia Waziri Ummy alitaka kujua chanjo ya ugonjwa Ebola inachukua muda gani kuanza kufanya kazi baada ya mtu kuchanjwa ambapo majibu yalitolewa kuwa chanjo hiyo inaanza kufanya kazi baada ya siku kumi huku muda wake wa kumkinga mtu ukiwa bado katika utafiti.
Vile vile Waziri Ummy alitaka kupata ufafanuzi kuwa chanjo hiyo ni kwa ajili ya aina gani ya virusi vya Ebola na ufafanuzi ulitolewa kuwa chanjo hiyo ni kwa ajili ya kirusi cha Zaire ambacho kwa sasa ndicho kinachosababisha mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.