**********************
Mwandishi wetu, Arusha
Wanafunzi wasichana wanaosoma vyuo vikuu mkoani Arusha, wamezindua kampeni ya kutomokeza matukio ya udhalilishaji wasichana katika mitandao ya kijamii nchini.
Kampeni hiyo imezinduliwa katika mdahalo wa matumizi sahihi ya mitandao na fursa zinazopatikana ulioandaliwa na taasisi ya elimu ya uraia na msaada wa kisheria(CILAO) kwa kushirikisha Taasisi ya msaada wa habari kwa jamii za asili za wafugaji, wawindaji na waokota matunda(MAIPAC) na shirika la ustawi wa wanawake na watoto(WOSWELS),
Wanafunzi hao wameanzisha hashtag TokomezaUkatiliKwaWanawakeMtandaoni ambayo itatumika kusambaza ujumbe kupinga ukatili dhidi ya wanawake katika mitandao.
Wameeleza kuna ongezeko la matukio la ukatili dhidi ya wanawake katika mitandao ya kijamii jambo ambalo linapaswa kupingwa.
Ester Koka mwanafunzi wa chuo kikuu cha tumaini Makumira kitivo cha sheria, amesema matukio yanayoendelea katika mitandao ya kijamii yanafaa kukemewa kwani wasichana wanadhalilisha kwa kujua ama kutojua.
“sisi kama wasichana matukio haya tunaona kama ni ukatili dhidi yetu, kuna taarifa za kikundi cha watu kuendesha udhalilishaji huu kwa kuwashawishi wasichana kutokana na hali ngumu ya maisha tunaomba waache”amesema.
Anna levaan mwanafunzi wa chuo kikuu cha Makumira amesema kupitia mafunzo waliopata katika mradi wa uelewa masuala ya mtandao,wanaamini inawezekana kukomeshwa ukatili dhidi ya wanawake kama sheria za nchi na maadili yakifuatwa.
“kuna ambao wanapenda kusambaza picha zisizo na maadili lakini kuna ambao wanalazimishwa hivyo ni muhimu wanafunzi wakike kutumia vizuri mitandao,” amesema
Mtaalam wa masuala ya mitandao ya kijamii, Elie Chansa akitoa mada katika mdahalo huo, ulioandaliwa na Taasisi hizo ikiwa ni sehemu ya Mradi wa boresha habari unaofadhiliwa na shirika la internews kwa ushirikiano na shirika la misaada la marekani(USAID),lengo ni kubainisha fursa zilizopo katika mitandao ya kijamii ambazo zikitumiwa vizuri zitasaidia wanafunzi wa kike.
Amesema badala ya kutumia mitandao kusambaza mambo yasiyo na manufaa nimuhimu kuitumia mitandao kupata elimu, kupaza sauti juu ya ukatili lakini pia kufanya biashara na hivyo kujipatia vipato halali.