Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akutana na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa,anaye maliza muda wake hapa Nchini Tanzania Bw. Alvaro Rodriguez .kwa ajili ya kumuaga Waziri Mkuu ofisini kwake .Magogoni jijini Dar es Salaam.leo
……………..
UMOJA wa Mataifa (UN) umeipongeza Serikali ya Tanzania kwa namna inavyotumia vizuri rasilimali zake za ndani na hivyo kuiwezesha kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo sambamba na kupunguza utegemezi kutoka nje.
Pongezi hizo zimetolewa leo (Jumatano, Agosti 21, 2019) na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Bw. Alvaro Rodriguez alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ofisini kwa Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam.
Mratibu huyo Mkazi wa Umoja wa Mataifa ambaye alikwenda kumuaga Waziri Mkuu, amesema kuwa Tanzania imeendelea kutumia vizuri mapato yake ya ndani kwa kuimarisha miundombinu na huduma za kijamii kama ujenzi wa hospitali na vituo vya afya.
“Katika kipindi changu cha miaka mitano ambacho nimefanya kazi Tanzania, nimeshuhudia mabadiliko makubwa ya kimaendeleo yanayofanywa na Serikali, ikiwemo kuimarika kwa mahusiano kati ya Serikali na Umoja wa Mataifa na taasisi zake nchini.”
Katika hatua nyingine, Bw. Rodriguez ameisifu Serikali ya Tanzania kwa namna ilivyoweza kuandaa na kuendesha vizuri mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Agosti 17 na 18 mwaka huu.
Mbali na kuisifu Serikali pia kiongozi huyo amevipongeza vyombo vya habari kwa jinsi vilivyoshirikiana na Serikali kuripoti matukio mbalimbali ya mkutano huo. “Nawapongeza na wananchi kwa ushirikiano walioutoa kwa Serikali wakati wote wa mkutano wa SADC.”
Kwa upande wake, Waziri Mkuu amemshukuru kiongozi kwa pongezi alizozitoa ambazo ni ishara kwamba anatambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli katika kutumia vizuri rasimali zake.
Waziri Mkuu amesema “maelezo yaliyotolewa na Bw. Rodriguez yanaakisi kauli za Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwamba Tanzania si nchi masikini na inayo uwezo wa kutoa misaada kutokana na rasilimali nyingi ilizonazo. Watanzania waendelee kuiunga mkono Serikali yao.”
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza kiongozi huyo kwani alikuwa kiungo kizuri kabaina ya Serikali ya Tanzania na Umoja wa Mataifa. Pia atakumbukwa sana kutokana na mambo mengi aliyoyafanya kipindi cha utumishi wake nchini Tanzania.
Awali, Waziri Mkuu alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Balozi Thamasanqa Dennis Mseleku ambaye alikwenda kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi nchini Tanzania.
Waziri Mkuu alimpongeza Balozi huyo kwa ushirikiano na mchango alioutoa kwa Serikali ya Tanzania katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo zikiwemo za kiuchumi, elimu, afya, maendeleo ya jamii pamoja na kuimarisha uhusiano baina ya nchini mbili hizo.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi Mseleku ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa uliompatia katika kipindi chake cha utumishi akiwa nchini na kwamba alitamani aendelee kubaki Tanzania.