Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mandewa Hamisi Ireme akiongoza harambee y kwa ajili ya ujenzi wa darasa la shule ya awali ya Mwaja Kitope iliyofanyika jana. Kutoka kushoto ni mdau wa maendeleo wa kata hiyo Hamisi Msaghaa, Katibu wa CCM wa Kata hiyo Yusuph Kijanga na Mwenyekiti wa CCM Tawi la Mwaja Juma Asi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwaja John Pascal akizungumza kwenye harambee hiyo.
Harambee ikiendelea. |
Mwenyekiti wa CCM Tawi la Mwaja Juma Asi akichangiajambo kwenye harambee hiyo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
WANANCHI wa Mtaa wa Mwaja Kitope kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mandewa mkoani Singida wamefanya harambee kwa ajili ya ujenzi wa darasa la Shule ya Awali Kitope.
Kukamilika kwa darasa hilo kutawaondolea adha watoto wa eneo hilo ya kutembea umbali wa kilometa zaidi ya tatu kwenda kupata elimu Shule ya Msingi Mwaja.
Katika harambee hiyo iliyoongozwa jana na Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Mandewa Hamisi Ireme Jumla ya Sh.445,000 zilipatikana huku Sh.100,000 ikitolewa na Mbunge wa Singida mjini Mussa Sima.
Akizungumza baada ya kuongoza harambee hiyo Ireme alisema amefarijika sana kwa mwamko wa wananchi wa eneo hilo wa kupenda maendeleo kwani darasa la shule ya awali walilokuwa wakisomea watoto lilikuwa limechaa na kutofaa tena.
Alisema harambee hiyo imekwenda vizuri kwani wananchi wamechangia fedha, mchanga, saruji na mbao hivyo matarajio yao ni darasa hilo kukamilika haraka iwezekanavyo Januari mwakani na kuanza kutumika.
“Ili mtu aweze kuishi maisha mazuri ni lazima uwe na elimu ambayo unaipata kuanzia shule ya awali na ndio maana leo hii tupo hapa tukiwajengea watoto wetu mazingira mazuri ya kupata elimu ambapo watakuja kutusaidia baadae katika taifa letu” alisema Ireme.
Ireme alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi, viongozi wote wa CCM na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaunga mkono katika shughuli za maendeleo akijitolea mfano kwenye eneo lake ambapo Serikali imewapa Sh.120 Milioni kwa ajili ya kujenga madarasa sita Sekondari ya Mandewa.
Katibu wa CCM wa Kata ya Mandewa Yusuph Kijanga alisema maendeleo yoyote hayaji kwa siku moja hivyo aliwashukuru wananchi wa eneo hilo kwa kujitokeza kwenye harambe hiyo ambapo wanaunga mkono jitihada za Serikali inayoongozwa na Rais Samia ya kuhakikisha watoto wanapata elimu bure kuanzia shule ya awali hadi sekondari.
” Hata hapa tulipo kati yetu hakuna mtu aliyejikamilisha kwa kuwa na choo, jiko, stoo, bafu na vitu vingine hivyo tunapaswa kuwa wavumilivu na kuacha kubeza jitihada za maendeleo zinazofanyika ” alisema Kijanga.
Alisema Serikali ya CCM ni sikivu na inaangalia mahitaji kulingana na kipaumbele hivyo ni vizuri kuiunga mkono kwa kufanya kazi kwa bidii.
Mjumbe wa kamati ya siasa wa kata hiyo na mdau wa maendeleo Hamisi Msaghaa ‘maarufu Dalali Muna’ alisema ni aibu kuona watoto wa eneo hilo wakiteseka kwenda kupata elimu mbali wakati wazazi wapo hivyo alitoa wito kwa wazazi kujitokeza kujenga darasa hilo haraka iwezekanavyo na yeye atachangia mbao zote za kupaulia jengo hilo.
Mkazi wa eneo hilo Fatuma Mlangida alisema kuna kila sababu ya kuongeza nguvu ya pamoja ili kuwanusuru watoto hao kwani darasa lao walilokuwa wakilitumia limechakaa na ametumia fursa hiyo kuwaomba wadau wengine wa maendeleo kuwaunga mkono.
Mwalimu wa watoto hao Yona Mathias alisema amekuwa akiwafundisha watoto hao kwa zaidi ya miaka saba na kama wananchi wa eneo hilo wangeanza mapema ujenzi huo tayari wangekuwa na madarasa saba kwani watoto hao sasa wamehitimu darasa la saba.
Alisema tangu ameanza kuwafundisha watoto hao mwaka 2015 watoto 196 walienda kuanza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mwaja.