*****************************
Adeladius Makwega
Dodoma
Katika makala yangu iliyotangulia nilikusimulia namna Wazaramo wanavyowaogopa Wazigua kwa ushirikina lakini leo hii nalitazama kabila la Wadigo ambao wapo jirani na Wazigua ambapo Wadigo hao pia wanautani na Wanyamwezi.
Kuufahamu utani kwa kabila la Wadigo nilijaribu kutazama kwa kina maana ya neno lenyewe Utani ndani ya WADIGO yake. Neno hilo hutamkwa kama UHANI na linatajwa sana katika matamshi ya kabila la Wadigo, mtu anayefanya Uhani huitwa MHANI na mtu anayeshiriki huitwa KUHANI ambapo kwa muelekeo wote huo ndipo neno UTANI huibuka.
Katika kabila la Wadigo wako watu wenye ubini huo MHANI ambapo pengine wakizaliwa na mzazi mmoja kutoka kabila la watani la Wadigo kama vile Wazaramo, Wanyamwezi au Wasegeju.
Kwa kidigo KUHANI maana yake kusaidia. Kwa watani wa wadigo kumekuwa na desturi ya kutaniana mathalani Mdigo hufika nyumbani kwa mtani na kumwambia nimekuja nimesikia umekufa, nimekuja kurithi lile dume la Mbuzi lililonona. Anayetaniwa huibuka na kusema ni kweli nimekufa lakini ukimchukua beberu langu na kulichinja majini yangu yatakuwa yametoka kwangu na yatamuigia beberu huyu na ukimchinja majini hayo yatakuingia wewe utadhulika.
Inaaminika kuwa Wadigo wana utani na Wasegeju, Wazaramo na Wanyamwezi. Sababu kubwa na ya msingi ya utani baina ya Wasegeju na Wazaramo ni kwa hali ya kupakana kwa makabila jirani tu.
Hoja ya msingi na ya kujiuliza ni je kwanini Wadigo hao wanakuwa na utani na kabla ya Wanyamwezi ambao wapo umbali mrefu na wao? Hapo ndipo makala yangu kwa leo itajikita. Katika kabila la Wazigua wana ukoo unaofahamika kama Semani ukoo upo jirani na Wadigo kwa kuwa Wanyamwezi wana utani na Wazigua na Wazaramoni, utani wa Wanyamwezi na Wadigo inaaminika ulipitia ukoo huo wa Semani ambapo pia kuna akina Semani ambao ni Wadigo. Kwa hiyo Wanyamwezi walipofika Udigoni waliwalinganisha Wadigo na wazigua hapoa utani ukaendelea kama kawaida.
Lakini wapo wanaoamini kuwa utani baina ya Wadigo na Wanyamwezu ulipamba moto wakati wa ukoloni wakati wa kilimo cha Mkonge. Katika kabila la Wadigo kuna simulizi moja kuwa kuna wakati mmoja Mnyamwezi aliagizwa na Mdigo akamuangalie nazi zake katika kiunga chake.
Kweli Mnyamwezi alifunga safari hadi katika kiunga hicho cha minazi. Basi Mnyamwezi alichukua shoka na panga na akaza kukata minazi na kuiangusha chini na kwa kuwa Mnyamwezi alikuwa na nguvu sana hadi mwenye shamba huyu Mdigo anafika hapo shambani alikuta tayari nusu ya kiunga hicho cha minazi kimekatwa hivyo na jambo hilo lilimtia hasara mno Mdigo.
Mnyamwezi badala ya kuupanda mnazi na kuziagua nazi yeye akaikata minazi bila huruma na kuleta hasara kiungani kwa Mdigo. Jambo hilo lilijadiliwa kwa kina ilielezwa kuwa ni kweli Mnyamwezi amekosea lakini kwa kuwa Mnyamwezi ni mtani na Mdigo, Mdigo alishindwa kesi hiyo na Mnyamwezi aliendelea na maisha yake kama kawaida pale Udigoni.
Kwa kuwa aliyefanya hivyo alikuwa mtani hakukuwa na neno, Mnyamwezi huyo alisamehewa huku wakisema kuwa huyu mnyamwezi hafahamu vizuri mazingira ya wadigo.
Kazi ya Mnyamwezi ni kuutafuta mwezi tu na Wadigo walikuwa wakiamini kuwa kwa kuwa Wanyamwezi walishindwa kuupata huo mwezi mwisho wa siku wakawa na tabia ya kuvamia maeneo ya makabila mengine tu na ndiyo maana leo wapo katika miji ya watu. Hapo ndipo utani ukazidi baina ya Wadigo na Wanyamwezi.