********************************
KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA KUVUNJA STOO NA KUIBA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia ALLY MWAKISU [37] Mkazi wa Ndola kwa tuhuma za kuvunja Stoo usiku na kuiba mahindi gunia 20 na Maharage gunia 08.
Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 28.12.2021 majira ya saa 15:30 alasiri huko Kijiji cha Ndola, Kata ya Nsalala, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya katika Misako inayoendelea maeneo mbalimbali.
Ni kwamba mnamo tarehe 14.12.2021 majira ya usiku mtuhumiwa alivunja Stoo ya Mfanyabiashara aitwaye JANE MWANGAILE [28] Mkazi wa Ndola na kuiba mali hizo. Mtuhumiwa amehojiwa na kukiri kutenda kosa hilo. Msako wa kuwatafuta watuhumiwa wengine walioshirikiana nae unaendelea.
KUKAMATA POMBE KALI ZILIZOPIGWA MARUFUKU NCHINI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya mnamo tarehe 29.12.2021 majira ya saa 16:00 jioni huko Kyela kati, Kata ya Ndandalo, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya lilifanikiwa kukamata Pombe kali aina ya Win box 3, Caferhunm box 3, Ice box 1 na Zikomo box 01, zilizotengenezwa nchini Malawi ambazo zimekatazwa kuingizwa nchini Tanzania. Aidha tunaendelea na msako wa kumtafuta mtuhumiwa ambaye alikimbia baada ya kuwaona Askari na kutelekeza pombe hizo.
MGOGORO WA KANISA LA EATG – MBEYA.
Mnamo tarehe 28.12.2021 majira ya saa 19:00 Jioni huko katika kanisa la Evangelical Assembly of God Tanzania [EAGT] lililopo Ilemi “B” Jijini Mbeya kulitokea vurugu kati yaAskofu Mkuu wa Kanisa hilo Taifa BROWN MWAKIPESILE na timu yake kutoka Makao Makuu ya Kanisa Dodoma dhidi ya Waumini wa Kanisa hilo ambao walipinga aliyekuwa mke wa marehemu Askofu wa Kanisa hilo marehemu Mch.USWEGE MWAKAFWILA – mwanzilishi kuchukua nafasi ya Uaskofu Mkuu wa kanisa hilo.
Ni kwamba Mch.USWEGE MWAKAFWILA ambaye ndiye mwanzilishi wa kanisa hilo alifariki tarehe 30/01/2021 hivyo Maaskofu wa Jimbo walimteua Mch.FRANCIS JOSEPH MPOLE kuwa mchungaji wa kanisa hilo lakini mke wa marehemu SUMA MWAKAFWILA alipinga uteuzi huo kwa madai kuwa hakushirikishwa kwenye uteuzi huo.
Hivyo alikwenda kulalamika Makao Makuu ya Kanda ambapo hakusikilizwa na kupelekea kwenda Makao Makuu ya Taifa Dodoma ambapo alisikilizwa malalamiko yake na kuonekana na haki kutokana na katiba ya kanisa hilo kuonyesha yeye ndiye anastahili kuchukua nafasi ya Uchungaji wa kanisa hilo.
Siku hiyo ya tarehe 28.12.2021 Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Taifa BROWN MWAKIPESILE pamoja na timu yake walifika Mbeya na kufanya kikao ambacho kilitengua nafasi ya uchungaji wa FRANCIS MPOLE na kumteua SUMA MWAKAFWILA kuwa Mchungaji wa kanisa hilo hali iliyozua vurugu kutoka kwa waumini wa kanisa hilo hivyo Jeshi la Polisi lilifika na kurejesha hali ya amani na utulivu.
KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA MAUAJI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia UPENDO JAMES MWAKIFAMBA [21] Mhudumu wa Bar na Mkazi wa Lupa Market – Chunya kwa tuhuma za mauaji ya Mhudumu mwenzake wa Bar aitwaye HILDA IDD MWAMBONA [25] Mhudumu na Mkazi wa Kijiji cha Lupa Market – Chunya kwa kumkata na chupa tumboni.
Tukio hilo limetokea mnamo tarehe 30.12.2021 majira ya saa 04:00 alfajiri huko katika Kijiji cha Lupa Market kilichopo Kata ya Ifumbo, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Chanzo cha tukio hilo ni kugombania chenji Tshs.2500/= waliyoachiwa na mteja.
HILDA IDD MWAMBONA alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi muda mfupi baada ya kufikishwa Zahanati ya Kijiji cha Ifumbo kwa matibabu. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani.