******************
Na Kassim Nyaki, Dubai UAE.
Tanzania ni miongoni mwa Nchi 192 zinazoshiriki maonyesho ya dunia ya EXPO Dubai 2020 yanayofanyika katika Mji wa Dubai ulioko nchi ya Falme za Kiarabu.
Katika maeonesho hayo idadi ya wageni kutoka mataifa mbalimbali wanaotembelea banda la Tanzania imezidi kuongezeka kutoka wastani wa wageni 640 kwa siku mwezi oktoba 2021 hadi kufikia wastani wa wageni 3500 kwa siku ya jana tarehe 26 Desemba, 2021.
Mkurugenzi wa Banda la Tanzania katika maonesho hayo Bi. Getrude Ng’weshemi ameeleza kuwa ongezeko la wageni wanaotembelea banda hilo umetokana na Serikali ya Tanzania kundelea kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma mbalimbali katika banda hilo zinazohusu fursa zilizoko Tanzania katika Sekta za Utalii, Uwekezaji, Madini, Miundombinu ya Nishati, Utamaduni na uwepo wa Mlima Kilimanjaro.
“Kila nchi ina bidhaa ambazo imekuja kuzitangaza kwenye maonesho haya, Tanzania tuna mengi ya kuonesha pia kwa mfano uwepo wa fursa za uwekezaji, vivutio vingi vya utalii vilivyopo Tanzania Bara na Zanzibar, Ujenzi wa Miundombinu ya Kimkakati kama bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere, Miradi ya ujenzi wa reli ya kisasa pamoja na sifa ya Tanzania kuwa nchi pekee inayotoa madini aina ya Tanzanite duniani ni miongoni mwa vitu vinavyowavutia wageni kutembelea banda letu” aliongeza Bi Getrude.
Bw. Dirk engelhard raia kutoka Ubelgiji ambae ni miongoni wa Wageni waliotembelea banda hilo ameeleza kuwa moja ya sababu zilizomleta katika banda la Tanzania ni kupata maelezo kuhusu tukio la kuhama kwa Nyumbu kutoka Kenya hadi Tanzania ambao hutoka katika Hifadhi za Maasai Mara kuingia Serengeti hadi Ngorongoro na baadae kurudia njia hiyo.
“Nimekuwa nikisikia kuhusu tukio la kuhama kwa Nyumbu kutoka Kenya hadi Tanzania, nimeshapanga Safari ya kuja Tanzania mwezi Februari mwaka 2022 nimeona nitumie fursa hii kuja kupata maelezo ya ziada ili niweze kuandaa safari yangu pamoja na rafiki zangu nitakaoongozana nao” aliongeza Dirk.
Wageni kutoka mataifa mbalimbali katika maonesho hayo ambao baadhi yao wamewahi kutembelea Tanzania kwa nyakati tofauti wanaeleza kuwa Uwepo wa picha na taarifa za vivutio vya utalii vinavyoonesha Mlima Kilimanjaro, Zanzibar, Ngorongoro na Serengeti ni miongoni vya vituo vinavyowashawishi kutembelea banda hilo.
Miongoni mwa taasisi za Tanzania zinazoshiriki maonyesho hayo ni pamoja na Mamlaka ya maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Wakala wa Huduma za Misitu Tazania (TFS), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania uliopo Abu Dhabi katika Nchi ya falme za Kiarabu.
Maonesho hayo ya kimataifa yaliyoanza tarehe 01 oktoba, 2021 yanaendelea hadi mwishoni mwa mwezi Machi, 2022.