****************
MICHUANO ya mpira wa miguu maarufu kama ‘Mwenda Cup’ imezidi kushika kasi katika Uwanja wa Mikocheni ‘A’ baada ya hapo jana timu ya Wanyama kuizamisha timu ya Master Plan 1-0 na kufanikiwa kuingia fainali ya michuano hiyo.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Meya Mstaafu wa Manispaa ya Kinondoni Yusufu Mwenda chini ya Taasisi ya Mwenda Foundation, yalishirikisha jumla ya timu 16 huku leo ikitarajiwa kupigwa nusu fainali ya pili kati ya ‘Mkunguni dhidi ya Huruma si Malezi’ tayari kwa kuwapata wababe wataochuana hatua ya fainali
Mchezo baina ya Wanyam na Master Plan ulikuwa vuta nikuvute huku timu zote zikionyesha kiwango kizuri hadi Dakika ya 75 Wanyama walipofanikiwa kupata goli lao la kuongoza na ushindi na kuwatupa nje Master Plan katika mashindano hayo ambayo lengo lake ni kudumisha upendo na urafiki baina ya wachezaji na mashabiki wa mpira.
Awali akiizungumzia michuano hiyo mdhamini wake Yusuf Mwenda alisema pamoja na kudumisha upendo na urafiki, mashindano hayo pia yamelenga kuwahamasisha vijana hao na wengine kuendelea ‘kuchapa’ kazi ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan.
” Michezo ni furaha, michezo ni upendo, nimefurahi kwa namna ambavyo nyote mlivyoonesha ushiriki mzuri wakati wote na zaidi mlivyonesha na kudumisha amani tangu kuanza kwa mashindano haya” alisema Mwenda
Aidha alisema mipango yake ni kuona Mikocheni inakuwa na timu bora ya mpira wa miguu ambayo itadhaminiwa na taasisi hiyo ya Mwenda ambayo hapo baadae itashiriki michuano mbalimbali ya ngazi zote hadi Ligi Kuu,.
Pamoja na hilo alisema kupitia timu hiyo matarajio ni kuona vipaji mbalimbali vya wachezaji vinapatikana na kutangazwa ili waweze kupata nafasi katika vilabu mbalimbali vya ligi za ndani na nje ya nchini.
Bingwa wa mashindano hayo atashinda zawadi ya Pikipiki huku mshindi wa pili akiibuka na kiasi cha Sh Milioni 1, mshindi Sh 500,000 na mshindi wa nne akiibuka na kifuta jasho cha Sh 250,000 huku fainali ya mashindano hayo ikitarajiwa kufanyika Desemba 25 mwaka huu.