Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akipata maelezo kuhusu hatua za uchimbaji wa visima vitatu kwenye vijiji vya Mbugani, Ngh’ambi na Kiegea katika Wilaya ya Mpwapwa. Waziri Jafo ametembelea Wilaya ya Mpwapwa leo tarehe 23/12/2021 kukagua shughuli za mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mifumo ikolojia vijijini, ambapo kuna shughuli za uchimbaji wa visima, ujenzi wa josho, uchimbaji wa lambo na utengenezaji wa majiko banifu. Wengine katika picha, wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Bw. Josephat Maganga na Meneja wa Ruwasa Mhandisi Cyprian Warioba.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akikata utepe kuzindua josho la kuogeshea mifugo lenye uwezo wa kuhudumia mifugo 8,327 lililojengwa katika Kijiji cha Nghambi ikiwa ni moja ya shughuli zinazotekelezwa na Mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mifumo ikolojia vijijini ulipo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais na unatekelezwa katika Wilaya tano nchini ambazo ni Mpwapwa, Mvomero, Kishapu, Simanjiro na Kaskazini – A
*********************
Uongozi wa Wilaya ya Mpwapwa umepewa siku Arobaini na tano kukamilisha usimikaji wa mabomba na matanki ya kuhifadhi maji safi na salama kwenye vijiji vya Mbugani, Ngh’ambi na Kiegea katika Wilaya ya Mpwapwa.
Agizo hilo limetolewa leo Desemba 23, 2021 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua Utekelezaji wa Mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mifumo ikolojia vijijini ulipo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais na unatekelezwa katika Wilaya tano nchini ambazo ni Mpwapwa, Mvomero, Kishapu, Simanjiro na Kaskazini – A
Akiwa Wilayani Mpwapwa katika kijiji cha Nghambi Dkt. Jafo amekasirishwa na kitendo cha mkandarasi wa Kampuni ya Make Engineering kutoka Dar es Salaam kutokamilisha kwa wakati mradi wa uchimbaji wa visima vyenye urefu wa mita 150 na kumuagiza mkandarasi huyo kukamilisha kazi mapema iwezekanavyo.
Amesema azma ya Serikali ni kuhakikisha huduma zinasogezwa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.
“Natoa siku Arobaini na tano tu maji yaanze kutoka hapa, mradi huu ukamilike. Wananchi hawa wanataka maji mapema, hakuna kwenda sikukuu na watumishi acheni kukaa maofisini, simamieni hili kikamilifu” Alisisitiza Dkt. Jafo.
Aidha, ametoa rai kwa wakazi wa Mbugani, Ngh’ambi na Kiegea kutumia vizuri mvua zinazonyesha kwa kupanda miti kwa vingi ili kulinda mazingira, na kusisitiza kuwa agenda ya mazingira ndio kipaumbe cha Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Bw. Josephat Maganga amesema atahakisha ndani ya siku arobaini na tano kazi zote zinakamilika na huduma ya maji inatolewa kwa wananchi.
Mradi wa kuhimili badiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini unafadhiliwa na Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi kwa Nchi Maskini kupitia Mfuko wa Dunia wa Mazingira ambapo kuna shughuli za uchimbaji wa visima, ujenzi wa josho, uchimbaji wa lambo na utengenezaji wa majiko banifu. Miradi yenye jumla ya Tshs. 2,257,042,400/- imeidhinishwa kutekelezwa katika Wilaya ya Mpwapwa.