Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akifafanua jambo kwa Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Juma Kijavala, wakati alipofika majira ya usiku kukagua utendaji kazi wa Bandari hiyo.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akipitia taarifa ya meli zilizoingia Bandari ya Dar es Salaam kutoka kwa Meneja wa Bandari hiyo Bw. Juma Kijavala, wakati alipotinga usiku na kukagua utendaji kazi wa Bandari hiyo.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, akisisitiza jambo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Bw. Eric Hamiss (kushoto)na Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Juma kijavala (kulia), wakati alipofika wakati wa usiku katika Bandari hiyo kukagua utendaji kazi wake.
Kazi za upakuaji wa mizigo zikiendelea nyakati za usiku katika Bandari ya Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akikagua utendaji kazi wa Bandari ya Dar es Salaam, alipofanya ziara ya kushtukiza majira ya usiku na kutizama shughuli zinavyoendelea.
PICHA NA WUU
……………………………………………………………….
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amezitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Kitengo cha kuhudumia Makasha (TICTS), kujipanga vyema na kuongeza idadi ya watu katika usimamizi wa shughuli zote za upakiaji na upakuaji wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam.
Prof. Mbarawa ameyasema hayo jana usiku mara baada ya kukagua shughuli zinazofanywa na Mamlaka hizo katika Bandari hiyo masaa 24 na kubaini kuwepo kwa msongamano wa malori mengi wakati wa kuingia na kutoka bandarini.
Pamoja na mambo mengine Prof. Mbarawa amesisitiza umuhimu wa mawasiliano ya mara kwa mara katika taasisi hizo ili kuweza kupunguza changamoto zinazowakabili na kuongeza ufanisi wa bandari.
“Msongamano upo lakini unaweza ukatatuliwa vizuri kama kila mmoja akijipanga vizuri katika eneo lake na kuhakikisha kazi zinakwenda vizuri, mtambue fika kuwa bandarini sio sehemu ya kumpumzika” amesisitiza Prof. Mbarawa.
Aidha, Prof. Mbarawa amesema Serikali imekwishachukua hatua za mwanzo za kupunguza msongamano bandarini hapo kwani malori yote yanayobeba mafuta yameruhusiwa kupita bila ya kupima na kuna vituo maalum ambavyo vimewekwa kwa ajili ya malori hayo.
“Serikali imekwisha punguza msongamano humu na sasa inataka kwenda mbele zaidi hata magari yote yanayoenda bandari kavu yasipime humu ndani ili kuendelea kupunguza msongamano”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Waziri Mbarawa, amekerwa na tabia ya mawakala wa mizigo (Agents) kutokukamilisha taratibu zote za vibali kwa wakati na hivyo kusababisha malori kukaa bandarini hapo wakisubiria kwa muda mrefu.
“Kwanzia sasa lazima magari yanayoingia bandarini yawe na vibali vya kutosha, hapa sio mahali pa kukaa na kulala siku tatu au nne, hakikisheni mnawachukulia hatua kali mawakala wote hata kama ni kufutiwa leseni zao katika ucheleweshaji wa vibali kwani wao ni tatizo kubwa bandarini hapa”, amesema Prof. Mbarawa.
Hata hivyo amewapongeza TPA kwa kazi kubwa wanayoifanya kwani mzigo ni mwingi na meli zilizoko nje zinasubiria kuingia ni nyingi na kuwataka kuendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha hakuna kinachoharibika na kuendelea kuingizia mapato nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Eric Hamiss, ameeleza kuwa wamepata baraka ya kupata mizigo mikubwa sana katika bandari ya Dar es Salaam kwani nje kuna meli 18 zinasubiria kuingia na ndani meli 13 zinaendelea kushusha mzigo na kazi zinaendelea masaa 24.
Ameishukuru Serikali kwa kuruhusu malori yanayobeba mafuta kutopima katika mizani bandarini hapo na kwa hali ya hivi sasa foleni imepungua kwa kiasi kikubwa.
Kuhusu suala la malori yasiyo na vibali, Bw. Erick ameeleza kuanzia Januari Mosi mwakani hakutakuruhusiwa malori kuingia bandarini hapo kama wakala hajakamilisha taratibu zote za vibali.
“Tutahakikisha kuwa tunayatoa malori yote yaliyopo ndani ya bandari ambayo hawajakamilisha vibali na kuruhusu wale tu wenye vibali kuingia”, amesisitiza Bw. Eric.