………………………………………………………………………
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wamemtaka mkandarasi wa uzoaji taka kuyapitia maeneo yote aliyoigia mkataba na Halmashauri ili kutimiza wajibu wake katika usafi wa mazingira.
Hayo yamebainishwa kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa wa Dome kata ya Ndembezi ambapo usafi wa mazingira imekuwa ni moja ya ajenda zilizozungumziwa na wananchi hao, maafisa wa idara ya afya na usafi wa mazingira, pamoja na mkandarasi wa uzoaji taka katika Manispaa ya Shinyanga.
Wananchi hao wamepongeza hatua hiyo ya utunzaji wa mazingira ambapo wamemtaka mkandarasi huyu kuyafikia maeneo yote na kuzoa taka kwa wakati ili kuweka mazingira katika hali ya usafi.
Akijibu maswali ya wananchi hao mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Networking Group iliyochukua tenda ya uzoaji taka Vitalis Alley amesema licha ya changamoto kadhaa anazokabiliana nazo kutokana na Jiografia ya maeneo lakini amekubali kuyafikia maeneo yote kwa ajili ya kuzoa taka kama sehemu ya wajibu wake.
“Kila Ijumaa tunaratiba katika mtaa huu wa Dome lakini ratiba zetu pia zipo katika ofisi za serikali za mitaa pamoja na ofisi za watendaji wa kata sisi changamoto kama hizi tunazipokea kama fursa na tunakwenda kuzifanyia kazi baada ya muda mfupi changamoto hizi zitakwisha huu ni mwanzo tu Jiografia ya maeneo haya imetuijia ugumu kidogo ndiyo maana kunakuwa na hizo changamoto lakini tunaahidi kupitia mkutano huu hizi changamoto tunakwenda kuzifuta moja kwa moja”.
Kwa upande wake mkuu wa idara ya usafi na mazingira Manispaa ya Shinyanga Kuchibanda Snatus amewaeleza wananchi kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira na taratibu za uzoaji taka zitakazofuatwa.
“Maguba yalikuwemo kwa ajili ya kutunza taka kwa muda wakati Halmashauri zinatafuta wapi pakupeleka kwa sababu hazikuwa na maeneo rasmi ya kutupa taka baada ya Halmashauri kujenga dampo ambalo lipo kwenye kata ya Kizumbi na kwa sababu sasa Halmashauri inaeneo la uhakika la kutupa taka kwahiyo hakuna sababu ya kuendelea kutumia maguba yale maguba yote mnayoyaona tunayafunga tutayabadilishia matumizi”.