……………………………………………………………………..
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Jamii imetakiwa kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kwenye vyombo vinavyohusika kuanzia ngazi ya serikali za mitaa, dawati la jinsia la jeshi la polisi pamoja na idara ya ustawi wa jamii.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa mtaa wa Dome Solomon Nalinga kwenye mkutano wa hadhara ambao pamoja na mambo mengine suala la ukatili wa kijinsia lilijadiliwa.
Nalinga amewakumbusha wananchi hao kutoa taarifa zenye viashiria vya ukatili wa kijinsia kama sehemu ya jitihada za kupunguza au kutokomeza vitendo vya aina hiyo katika jamii.
“Suala la ukatili wa kijinsia limekuwa likijitokeza mara kwa mara kwa baadhi ya familia au baadhi ya watu kwahiyo vunjeni ukimya ili suala la wote ukatili wa kijinsia ni mbaya kwa sababu unamtendea mwenzako jambo ambao haustahili kufanyiwa kadiri wewe linavyokuumiza na mwenzako linamuumiza hivyohivyo lakini pia tunawaomba kama kutakuwa na viashiria vyovyote vya ukatili katika ngazi ya familia iwe baba, mama au mtoto leteni taarifa hizo kwenye uongozi wa serikali ya mtaa”.
Mwenyekitu huyo pia amewakumbusha wananchi kuwa mabarozi wazuri katika suala la usalama wa maeneo wanayoishi ili kudhibiti mianya inayoruhusu kufanyika uhalifu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za Krismas na Mwaka mpya.
“Kila mwananchi awajibike katika suala la ulinzi na usalama na kutoa viashiria vyote kwenye serikali ya mtaa na sisi tutahakikisha tunatoa ushirikiano kwa ajili ya kuhakikisha kuwafichua watu wanao leta uvunjifu wa amani katika mtaa wetu lakini pia tunawaomba wakazi wote wa mtaa wa Dome na tunajiandaa na sikukuu tunawashauri siku za mikesha msiondoke nyumbani wote hakikisheni mnaacha watu na msiache vyitu ovyo nje”.
Kwa upande wao wakazi wa mtaa wa Dome wameipongeza serikali ya mtaa wao kwa kuwa na uongozi shirikishi ambao unawapa fursa ya kujadili masuala ya maendeleo kupitia mikutano ya hadhara ambapo pia wameliomba jeshi la polisi kuendelea kuimarisha ulinzi hasa katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za Krismas na Mwaka mpya.