Waziri wa mifugo na uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki wa kushoto akimkabidhi kitabu cha mwongozo huo Mkuu wa Mkoa wa Pwani wa kulia Mhe. Abubakari Kunenge katika halfa hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
*************************
VICTOR MASANGU, PWANI
Waziri wa mifugo na uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amezindua rasmi mwongozo wa upatikanaji na usimamizi endelevu wa maeneo kwa ajili y a marisho kwa mikoa sita na kusema kwamba serikali itatenga maeneo maalumu kwa ajili ya marisho kwa mifugo ya aina mbali mbali ili kuondokana na migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa halfa y uzinduzi huo ambao ulihudhuliwa na viongozi mbali mbali wa serikali, wakurugenzi, wakuu wa wilaya, viongozi wa dini pamoja na wakuu wa mikoa ipatayo sita ikiwemo Ruvuma, Mbeya , Manyara,Katavi , Morogoro, pamoaja na Mkoa wa Pwani ambao ndio ulikuwa ni mwenyekiti .
Waziri huyo alibainisha kwamba lengo kubwa la serikali la kuzindua mpango huo ni kwa ajili kuwa na upatikanaji wa maeneo ya marisho ya kisasa na uhakika ambayo yatakuwa yakihifadhi mifugo ya aina mbali mbali na kwamba jambo hilo litakuwa ni endelevu kutokana na kuweka mipango madhubuti ya kuwasaidia wafugaji waweze kufuga kwa kisasa zaidi.
Kadhalika Mashimba aliongeza kuwa lengo limgine la kuzindua mpango huo ni kumaliza kabisa migogoro iliyopo na kubainisha kwamba kwa sasa kuna changamoto kubwa ya uwepo wa mifugo mingi zaidi kuliko idadi ya watu hivyo kupelekea hata baadhi ya wafugaji kukosa kabisa maeneo ya kulishia na kuamua kwenda katika mikoa mingine kujitafutia sehemu.
“Ndugu zangu kwa sasa idadi wa mifugo iliyopo Tanzania ni mingi sana uukilinganisha na idadi ya watu kwa hiyo kwa maana hii katika siku za mbele tutakuwa katika wakati mgumu kutokana na mifugo inazidi kuongezea kila siku lakini ssuala la ardhi lenyewe aliongezeki kwa hiyo nina imani tukiutekeleza mpango huu vizuri tutaweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuthibiti ufugaji holela na kuingia katika ufugaji wa kisasa,”alibainisha Waziri Mashimba.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe.Abubakari Kunenge amebainisha kuwa kuzinduliwa kwa mpango huo kutakuwa ni mkombozi mkubwa kwa jamii ya wafugaji kuwaondolea kero cha changamoto mbali mbali amabzo zilikuwa zinawakabili katika suala zima la kupata maeneo ya kuweza kulishia mifugo yao.
“Napenda kuchukua fursa hii kukupongeza Waziri kwa kuweza kuja katika Mkoa wetu wa Pwani na mpango huu kwa upande wetu utakwenda kuwasaidia wafugaji wote katika maeneo mbali mbali ambao walikuwa wanateseka, lakini kitu kingine eneo hilo la sekta ya ufugaji kwetu ni muhimu sana katika kukuza suala la kiuchumi hivyo wafugaji na watumiaji wengine ambao wanatumia ardhi jambo hili linakwenda kutafutiwa ufumbuzi,”alisema Kungenge.
Aidha alifafanya kwamba serikali ya Mkoa wa Pwani walishakwenda na kukutana na jamii ya wafugaji na wakulima kuhusiana na kujadili juu ya migogoro iliyopo na wamesema kuwa wapo tayari kubadilika na kwamba serikali itaendelea kuwawekea mazingira mazuri ya kuwasaidia kwa hali na mali ili kuwaondolea migogoro iliyokuwepo.
Pia Kunenge alitumia fursa ya uzinduzi huo kueleza kuwa tayari Mkoa wa Pwani wameshaandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa lengo la kuweza kuepusha migogoro ya ardhi na kwamba itasaidia kuleta hali ya amani na utulivu katika maeneo yetu na kueleza bado wanaendelea kujitahidi kutoa elimu juu ya matumizi bora ya ardhi.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Abdala Ulega Naibu waziri wa mifugo na uvuvi Mhe.Abdalah Ulega amebainisha kwamba uzinduzi wa mpango huo utaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kuleta mabadiliko na neema kwa wafugaji wote kutokana na kuwepo na sehemu maalumu ya kwa ajili ya marisho ya mifugo yao.
“Kimsingi kwanza kabisa napenda kumshukuru kwa dhati Mkuu wa Mkoa wa Pwani kwa kuweza kukubali kufanyia halfa hii ya uzinduzi wa mpando kwa ajili ya marisho na mimi nina imani kubwa utapunguza migogoro ambali ilikuwa inajitokeza kwa wafugaji wa Mkoa wa Pwani pamoja na mikoa mingine ya Tanzania itaweza kusaidia katika suala zima la utekelezaji,”alisema Ulega.
Nao baadhi ya wakuu wa Mikoa sita ambao waliweza kuhudhulia katika uzinduzi huo wamesema mpango huo unatakiwa ufanyiwe kazi zaidi ili kuweza kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa kuwasaidia wafugaji kupata maeneo maalumu ambayo pia itaondosha kuwepo kwa migogoro.