Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Asia Messos (kulia) akizungumzia kuhusu ujenzi wa Zahanati ya Kisuluiga iliyopo Kata ya Gumanga ambapo Waziri Ummy ameagiza Halmashauri hiyo itoe Sh.60 milioni ili kukamilisha ujenzi wake.
Na Dotto Mwaibale, Mkalama
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Ummy Mwalimu amewataka Wananchi wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida kuzitunza barabara zilizojengwa na Serikali kwa gharama kubwa.
Ummy ametoa ombi hilo wakati akizungumza na wananchi hao wakati akikagua barabara ya Singa- Kinampundu-Ilunda iliyojengwa kwa kiwango cha changarawe katika ziara ya kikazi ya siku moja wilayani humo ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Jambo lililokubwa nawaomba wananchi mzitunze hizi barabara kwa sababu Serikali inazichonga lakini kunawananchi wanapitisha majembe ya kukokotwa na ng’ombe kwa hiyo niombe ulinzi wa barabara uwe ni jukumu letu sote kwa sababu fedha zilizotumika kuzitengeneza ni nyingi hivyo tunatamani ziendelee kuwa na ubora na zisaidie kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi” alisema Waziri Ummy.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijiji wa Wilaya ya Mkalama, Edward Masola alisema matengenezo ya barabara hiyo yatagharimu kiasi cha Sh.milioni 91,201,000.
Alisema barabara hiyo ambayo inaunganisha Kata za Ilunda na Kinampundu itakapokamilika itarahisisha usafiri kwa wananchi kufikia huduma za elimu, afya na masoko.
Katika hatua nyingine Waziri Ummy amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida kusaini mikataba yote ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Ilunda baada ya kuwepo madai ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo kugoma kuisaini kufuatia mgororo wa kugombea sehemu ya kujengwa kituo hicho ambapo baadhi ya madiwani walitaka kijengwe Gumanga.
Awali akitoa taarifa ya kituo hicho cha afya, Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Ibrahim Pazia alisema fedha za ujenzi wa kituo hicho ni Sh.250,000,000 zilizotokana na tozo na kuwa kitakuwa na majengo matatu jengo la wagonjwa wa nje (OPD) jengo la maabara na kiteketeza taka.
Alisema mradi huo utakapo kamilika utahudumia wananchi 12,000 wa vijiji vya Asanja, Nkungi, Ilunda na Iambi, Kinambili, Nduguti na vijiji jirani vya Mkunguru, Kidigida na Kata ya Kinampundu.
Waziri Ummy alitumia nafasi hiyo kuwaomba waheshimiwa madiwani kuacha mivutano ambayo haina tija ambayo inakwamisha maendeleo ya wananchi kama ilivyotokea katika kata hiyo.
Katika ziara hiyo Waziri Ummy alitembelea na kukagua kikundi cha Vijana cha Iguguno Youth Group kinachojishughulisha na ufyatuaji wa matofali na ufugaji wa kuku wa kienyeji ambapo aliwaunga mkono kwa kuwachangia Sh.2,000,0000 ambapo pia Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge aliwachangia kiasi hicho cha fedha.
Aidha Waziri Ummy alitembelea na kukagua darasa moja la Uviko-19 kati ya saba la Shule ya Sekondari ya Gumanga ambayo yamejengwa kwa Sh.140,000,000.