Na Dotto Mwaibale, Singida
MWENGE wa Uhuru unaotarajiwa kuwasili wilayani Ikungi mkoani Singida kesho asubuhi utazindua miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 1.162 .
Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo Edward Mpogolo (pichani) wakati akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu ukimbizaji wa mwenge wa Uhuru katika wilaya yake.
Mpogolo alisema mara baada ya kuwasili kwa mwenge huo na kupokelewa Kijiji cha Mkiwa patazinduliwa madarasa mawili ya Shule ya Msingi Darajani na kisha kuelekea kutembelea mradi wa upimaji wa virusi vya na elimu ya uchaguzi wa Serikali za mitaa uliopo katika Kijiji cha Issuna.
” Baada ya kutembelea mradi huo wa kijiji cha Issuna watakwenda kuweka jiwe la msingi ujenzi wa mnara wa kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere utakao jengwa Ikungi mjini” alisema Mpogolo.
Alisema baada ya hapo watakwenda kuweka jiwe la msingi wa mtandao wa maji Kijiji cha Ighuna pamoja na kutembelea mapambano dhidi ya dawa za kulevya Kituo cha Polisi cha Puma.
Aliongeza kuwa baada ya hapo watakwenda kukagua ujenzi wa Kituo cha Afya cha Sepuka na kufuatiwa na usomaji wa risala ya utii eneo la mkesha wa mwenge Uwanja wa Ofisi ya Mtendaji Kata ya Sepuka.
Mpogolo amewaomba wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kuupokea mwenge huo na kushuhudiwa miradi hiyo itakapo kuwa ikizinduliwa.