Mkuu wa Mkoa wa Kigoma akifungua kongamano la kupinga ukatili katika kampeni ya “Twende pamoja, ukatili sasa basi” lililofanyika Mkoani Kigoma kwa lengo la kujadili namna ya kutokomeza ukatili Mkoani hapo.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Mwajuma Magwiza akieleza lengo la kongamano la kupinga ukatili katika “Kampeni ya twende pamoja ukatili sasa basi” lililofanyika Mkoani Kigoma.
Mmoja wa washiriki wa Kongamano la kupinga ukatili ikiwa ni sehemu ya “Kampeni ya twende pamoja ukatili sasa basi”wakichangia mada kuhusu changamoto ya ukatili Mkoani Kigoma.
Mwanasheria na Mwandishi wa kitabu cha Mirathi na wosia Mhe. Jonathan Mgongoro akiwasilisha mada kuhusu nafasi ya Mwanamke na mtoto katika mirathi kwenye Kongamano la kupinga ukatili ikiwa ni sehemu ya “Kampeni ya twende pamoja ukatili sasa basi”wakichangia mada kuhusu changamoto ya ukatili Mkoani Kigoma.
…………………………………………………………….
Na WAMJW, Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andenge amesema kuongezeka kwa vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto vinarudisha nyuma jitihada za Serikali kufikia uchumi wa juu kutokana na Jamii kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu madhara yake.
Mhe Andengenye ameyasema hayo akifungua kongamano la Kampeni ya twende pamoja kupinga ukatili wa kijinsia lililofanyika Mkoani Kigoma ambapo amebainisha kuwa ili kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa juu, unaotegemea viwanda ni muhimu kuwepo na ustaarabu ikiwemo kuheshimu utu wa mtu.
“Hata tukiendelea kujenga reli, shule, hospitali katika mahali ambapo utu wetu unadhalilishwa na kundi moja dhidi ya kundi lingine vitu vyote hivyo vitakuwa havina maana” amesema Andengenye.
Ameongeza kwamba uchumi utakuwa wa maana kama utaonesha ustaarabu na Ustawi wa watu wanaonufaika na uchumi huo kw a kukemea vitendo vya ukatili kwa wanawake na Watoto ili vitokomezwe kabisa.
“Ukatili hasa wa kijinsia una madhara makubwa hata kufikia wanawake kutoshiriki shughuli za ujasiriamali na tunafahamu hapa Kigoma nguvu kazi kubwa ni wanawake hivyo nguvu hii lazima ilindwe kwa nguvu zote” amesema Andengenye.
Amesema iwapo Jamii inataka watoto wasome, wawe na afya njema na maadili ni lazima kuanza mapambano ya kuwalinda wanawake na Watoto kwa nguvu zote ili kupata wataalamu wa hapo baadaye.
Mkuu huyo wa Mkoa ameendelea kubainisha sababu za vitendo vya ukatili kuwa vinachangiwa na ukosefu wa elimu katika Jamii kuhusu Jinsi na Jinsia, Mila na Desturi kandamizi pamoja na umaskini hivyo kupelekea utumikishwaji wa watoto na kulazimishwa kuolewa katika umri mdogo.
Andengenye amesema Kampeni ya Twende pamoja inamgusa kila mwananchi kwani ukatili unafanyika katika maeneo mbalimbali kuanzia nyumbani, shuleni, maeneo ya wazi na kazini na wakati mwingine unafanywa na watu walioaminiwa.
“Ni jukumu letu sote kuhakikisha tunatoka taarifa ya matukio ya ukatili na unyanyasaji kwa wanawake na Watoto katika Mamlaka za Serikali na Polisi na kuhudhuria katika vituo vya kutolea Huduma za afya kwa wakati. Hakuna jambo rahisi ambalo tunarithisha kwa vizazi vijavyo kama ukatili. Katika hali yoyote ukatili ukifanyika tusipoukemea tujue kizazi kitakachokuja kitakuwa na uwezo na nguvu zaidi wa kufanya ukatili kuliko sisi”. Ameongeza Mhe. Andengenye
Amesema mijadala inayoibuliwa iwe kichocheo cha kuongeza nguvu katika kupambana na vitendo hivyo.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mwajuma Magwiza akiwasilisha lengo la kongamano hilo, amesema tangu mwaka 2018 Serikali ilipozindua MTAKUWWA lengo lilikuwa kupunguza ukatili kwa wanawake na Watoto kwa asilimia 50 lakini kupitia mijadala hii itasaidia kupunguza zaidi idadi hiyo.
“Serikali imeendelea kuratibu na kuunda kamati mbalimbali za ulinzi wa watoto na wanawake na hadi sasa kamati 18,186 kati ya 20,750 zinazotakiwa kuundwa katika ngazi zote” amesema Magwiza.
Aidha, pamoja na jitihada nyingine, Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka za Mahakama imesimamia kuhakikisha kesi za ukatili zinasikilizwa kwa muda mfupi kwa kuweka ukomo wa miezi 6.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Kigoma Nyamara Elisha akiwasilisha utekelezaji wa MTAKUWWA na mikakati iliyopo amesema mkoa umeunda
kamati za ulinzi wa mwanamke na mtoto 630 sawa na 100% pamoja na vikundi vya malezi chanya.
Naye mmoja wa washiriki wa Kongamano hilo Martha Jerome amesema wanajamii wenyewe ndiyo wanaofanya ukatili, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kukemea vitendo hivyo kwa kutoa taarifa na kuwa tayari kutoa ushahidi.
Kongamano hilo likiwa ni sehemu ya Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto yaani MTAKUWWA, limehusisha washiriki kutoka makundi mbalimbali kwenye Jamii Mkoani Kigoma ikiwemo Viongozi wa dini, wanazuoni, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, wajasiriamali, watoa huduma ngazi ya Jamii, wajumbe wa Kamati za MTAKUWWA, Walimu, wamiliki vyombo vya usafiri, Waganga wa tiba asili, wanahabari, Wazee maarufu, watu mashuhuri, Maafisa Maendeleo na Maafisa Ustawi wa Jamii.