Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa Jubilee Life Insurance, Karim Jamal wakitiliana saini ya ushirikiano wa kuzindua mpango wa Bima kwa ajili ya watu wa kipato cha kati na wafanyabiashara nchini uitwao, NMB FANAKA PLAN uliofanyika Dar es Salaam leo. Wanaoshuhudia kutoka kulia ni Mkuu wa Idara ya Bima NMB, Martine Massawe na Mkuu wa Idara ya Bima kwa Mabenki wa Jubilee Life Insurance, Dereck Rwezaura.
Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa Jubilee Life Insurance, Karim Jamal wakibadilishana nyaraka baada ya kutiliana saini makubaliano hayo.
Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa Jubilee Life Insurance, Karim Jamal wakionyesha nyaraka walizotia saini.
***************************
NA MWANDISHI WETU
BENKI ya NMB kwa kushirikiana na Jubilee Life Insurance, imezindua mpango wa utunzaji, uwekezaji na bima uitwao ‘Fanaka Plan,’ ambao licha ya kulinda maisha ya mteja aliyedhurika, pia unampa faida tele na uhuru wa kutunza fedha kwa utaratibu na muda atakaochagua.
Uzinduzi wa Fanaka Plan umefanyika jijini Dar es Salaam leo, ambako Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi na Mkurugenzi Mkuu wa Jubilee Life Insurance, Karim Jamal, walitiliana saini na kuutaja mpango huo kuwa ni kwa Watanzania wote – wenye akaunti NMB na wasio nazo.
Akizungumza kabla ya kuzindua mpango huo, Mponzi alisema Fanaka Plan ni mshirika sahihi wa watu wenye malengo ya muda mrefu na ya kati katika kujiimarisha kiuchumi na kufikia malengo binafsi, uwekezaji ukiwa ni wa kati ya miaka mitano hadi 20.
“Fanaka Plan” Ni uwekezaji ambao unakuwa na bima ya maisha kwa mteja. Hii inawawezesha Watanzania kuweka akiba kila mwezi katika vifurushi mbalimbali, ambavyo vinatoa faida kuanzia Sh. Mil. 5 na kuendelea, huku mteja akitakiwa kuchagua kifurushi ama ‘Plan’ kulingana na uwezo wake wa kuchangia kila mwezi.
“Hii maana yake utakuwa unajiwekea akiba, pesa yako itakupa bonasi na ikitokea mteja akapata ulemavu wa kudumu kabla ya wakati aliopanga, NMB na Jubilee Life tutalipa mchango wa miezi 36 (miaka mitatu), hata kama mteja alilipia miezi miwili tu na ikitokea akafariki, atalipwa bima kamili sawa na kifurushi alichochagua,” alisisitiza Mponzi.
Alibainisha kuwa, licha ya faida hizo kwa watakaopata ulemavu wa kudumu ama kifo wakiwa kwenye Fanaka Plan, mteja atakayemaliza muda aliochagua bila kupata ulemavu ama kifo, atalipwa kifurushi chake chote na atakuwa na bima ya maisha hadi atakapofikisha umri wa miaka 90 bila kuchangia kiasi kingine.
Aliwataka Watanzania kufika kwenye matawi ya NMB kote nchini, ili waweze kupata maelekezo muhimu ya namna ya kujiunga na Fanaka Plan, ambao aliutaja Kama mpango uliobeba Suluhu za changamoto zitokanazo na ukosefu wa uhakika wa kipato, lakini pia ukijihakikishia mwekezaji mnyororo sahihi wa mtiririko wa fedha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jubilee Life, Karim Jamal, alikiri kuwa wanajivunia aina ya ushirikiano uliozaa Fanaka Plan, ambao unazihusisha taasisi vinara – Kampuni yake ikiongoza miongoni mwa Kampuni za Bima Afrika Mashariki na NMB ambayo ni benki Bora na kinara wa taasisi za fedha Tanzania.
“Tunaishukuru NMB kwa aina hii ya ushirikiano chanya unaowahakikishia wateja usalama wa fedha na maisha yao, ushirikiano uliobeba tija na matarajio ya kesho iliyo njema kwa watoto na familia ya mteja iwapo atapata ulemavu ama kifo wakati akiwa ameshaanza kuwa mwekezaji kupitia Fanaka Plan,” alisema Jamal.
Jamal aliitaja Fanaka Plan kuwa ni mpango mzuri na wa aina yake, na kwamba kuenea kwa matawi ya NMB kote nchini na uzoefu mkubwa walionao wao katika nyanja ya Bima, unawapa Watanzania kimbilio sahihi lenye kila aina ya faida kwa vifurushi vyote na kwamba hakutakuwa na changamoto yoyote katika kupata huduma hiyo.