************************
NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
TAASISI ya The Desk & Chair Foundation (TD&CF) imekabidhi misaada ya vifaa saidizi,mitaji na vyerehani vya ushonaji kwa wajasiriamali wanawake,watoto wanne na watu wenye ulemavu kikiwemo Kituo cha Yatima cha Hekima Foundation,vyote vikigharmu sh.milioni 9.7.
Vyerehani hivyo 20 vilikabidhiwa kwa wanawake wajasirimali wadogo 19 na kituo cha watoto yatima cha Hekima Foundation,wilayani Nyamagana,viwasaidie kuingiza vipato na kuendesha maisha na familia zao na kujikwamua na umasikini.
Pia ilikabidhi vifaa saidizi (baiskeli) kwa watoto wenye matatizo ya migongo,watu wawili wenye ulemavu wa miguu na mitaji ya biashara kwa Asia Patrick aliyekatika vidole kwa ajali pamoja na Bora Said waingize vipato na kuwarahisishia kuboresha maisha yao.
Akizungumza jana wakati wa kukabidhi msaada huo,Mwenyekiti wa taasisi hiyo,Alhaji Sibtain Meghjee,alisema vyerehani hivyo vipya vitawasaidia wajasiriamali hao kuingiza vipato na kuboresha maisha yao na familia.
Alisema vifaa saidizi vya kuwarahisishia usafiri na maisha yao ambavyo ni baiskeli mbili kwa watu wenye ulemavu,watoto wawili wenye matatizo ya migongo walipewa viti maalumu na wengine wawili walipewa wheel chair,viwarahisishie usafiri kwenye maisha yao ya kila siku.
Alhaji Meghjee alisema taasisi hiyo iko bega kwa bega na serikali katika kuinua hali za maisha ya Watanzania wenzao wenye changamoto za kimaisha na inakabidhi msaada wa vifaa saidi na vya ushonaji vyenye thamani ya sh.milioni 9.72 kwa walengwa viwasaidie kuingiza vipato.
Aidha taasisi hiyo mbali na msaada huo inakarabati mfumo wa maji kwa kufunga pampu mpya ya kusukuma maji kutoka Ziwa Victoria umbali wa km 4 hadi kwenye Hospitali ya Bukumbi inayomilikiwa na Kanisa Katoliki mradi ambao umefikia asilimia 80.
Pia inaboresha mfumo wa maji wilayani Misungwi kwenye Makazi ya Wazee Bukumbi,kutoka kwenye kisima kifupi hadi kituoni hapo kwa ufadhili wa kikundi cha E NUDUBA cha mjini Toronto,Canada na kazi imefikia asilimia 50.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Amina Makilagi,akikabidhi misaada hiyo alisema,The Desk & Chair Foundation,inaisaidia serikali kuiwezesha jamii na wananchi kuondokana na changamoto za maisha.
“Serikali kwa upande wetu, The Desk & Chair Foundation ni kioo kwa miradi mnayofanya hapa mkoani Mwanza na Tanzania, mnaunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita na mmefanya jambo kubwa la kukumbukwa kwenye jamii,maana msaada huu haukuangalia dini,kabila wa rangi ya mtu almradi ni mhitaji,”alisema
Mkuu huyo wa wilaya alisema watu wenye ukwasi wa fedha hawafikirii kusaidia jamii zaidi ya kujirusha (kustarehe),hivyo waige shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo isiyo ya kiserikali.
Mikilagi alisema ushirikiano wa taasisi hiyo una tija kwa serikali katika kupunguza changamoto za jamii na kutoa rai kwa wajasiriamali waliopata vyerehani na mitaji waunde umoja au ushirika kwa mujibu wa sheria ili serikali iwawezeshe mikopo ya kukuza mitaji yao.
Baadhi ya wajasiriamali hao Penina Daud na Salome Kisura kwa nyakati tofauti waliishukuru The Desk & Chair kuwawezesha vitendea kazi hivyo bure,wengi hawakuwa na uwezo wa kununua zaidi ya kukodi vyerehani kwa sh.10,000 kwa mwezi wakaomba wafadhili kusaidia wengine wenye mahitaji ya aina hiyo.
Kisura alisema aliuza cherehani yake ili kupata fedha za kugharamia matibabu ya mume baada ya kuugua na kuishukuru taasisi hiyo kumwezesha kupata nyingine atakayoitumia kuingiza kipato.