KATIBU Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Desemba 19,2021 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya uzinduzi wa Kampeni-Jamii Shirikishi ya Pili dhidi ya Afua za Kinga ya UVIKO-19,utakaofanyika jijini Arusha Desemba 22,2021.
Baadhi ya waandishi wa habari pamoja na baadhi ya watumishi wa wizara ya Afya wakifatilia hotuba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi,(hayupo pichani) leo Desemba 19,2021 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu uzinduzi wa Kampeni-Jamii Shirikishi ya Pili dhidi ya Afua za Kinga ya UVIKO-19,utakaofanyika jijini Arusha Desemba 22,2021.
KATIBU Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Desemba 19,2021 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu uzinduzi wa Kampeni-Jamii Shirikishi ya Pili dhidi ya Afua za Kinga ya UVIKO-19,utakaofanyika jijini Arusha Desemba 22,2021.
………………………………………………………….
Na Alex Sonna, Dodoma
SERIKALI inatarajia kuzindua kampeni ya utekelezaji wa Mpango Shirikishi na Harakishi awamu ya Pili dhidi ya UVIKO-19 nchini Tanzania inayolenga kushirikiana wananchi na Wadau wa Maendeleo ili kuongeza chachu kwa watoa huduma ngazi ya Jamii kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari na kupata chanjo.
Akizungumza leo Desemba 19,2021 jijini Dodoma na waandishi wa habari , Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof.Abel Makubi, amesema uzinduzi huo utafanyika Desemba 22, mwaka huu jijini Arusha.
“Mtakumbuka kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliridhia matumizi ya Chanjo ya UVIKO-19 na mnamo tarehe 23 Julai, 2021, kwa mara ya kwanza Tanzania ilianza kutoa chanjo hizi za UVIKO-19 kwa kuanza na chanjo ya Jenssen, baadae Sinopharm na Pfizer. Aidha, hadi jana Tahehe 18 Desemba, jumla ya wananchi 1,275,795 sawa na 2.21% walikuwa wamepata chanjo kamili na kupata kinga kamili dhidi ya UVIKO 19, lengo la serikali ni kufikia 60% ya wananchi wote,”amesema.
Ameongeza “Ili kufanikisha malengo ya awamu ya pili na matumizi ya watoa huduma ngazi ya jamii, Wizara na OR-TAMISEMI imeandaa Mwongozo wa Wawezeshaji wa Wahudumu wa Afya ya Jamii ikiwa ni pamoja na kuwatambua Wahudumu waliopo katika ngazi ya Vijiji, Mitaa na Vitongoji na kuanza kuwajengea uwezo kwa kuwapatia mafunzo kuhusu kinga ya UVIKO – 19 na umuhimu wa wananchi kuchanja.”
Amesema katika Mikoa ya Mwanza, Dodoma, Manyara, Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, Songwe, Kilimanjaro, Geita, Ruvuma na Morogoro tayari Wahudumu zaidi ya 8,130 wamepatiwa mafunzo na wanaendelea na kazi ya uhamasishaji huku zoezi hili likiwa ni endelevu katika maeneo mengine nchi nzima.
“Katika Mpango Shirikishi na Harakishi awamu ya pili dhidi ya afua za kinga za kinga UVIKO-19, zinaelekezwa timu za afya katika Halmashauri na Mikoa kuendelea kuwatumia Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii ili kuendelea kuhamasisha na kuelimisha jamii juu ya hatua mbalimbali za kujikinga na UVIKO – 19 ikiwa ni pamoja matumizi ya chanjo,”amesema.
Amebainisha kupitia kampeni hiyo mambo yatakayozingatiwa ni Kuwezesha serikali za mitaa, vitongoji zenyewe kulisimamia zoezi hili la elimu na utoaji wa Chanjo na liwe endelevu (Kampeni ya Mtaa kwa Mtaa,na Kitongoji kwa Kitongoji), Kuendelea kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ili waendelee kutoa huduma ya chanjo kulingana na Miongozo ya nchi na Shirika la Afya Duniani, Waganga wa Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuongeza Vituo vya kutolea huduma za chanjo kulingana na mahitaji, zikiwemo huduma mkoba na kufungua vituo zaidi katika maeeeo ya mikusanyiko.
Pia Halmashauri zinatakiwa kuendelea kuwajengea uwezo Kata, Vijiji na Vitongoji katika kuelimisha jamii na kupeleka huduma za chanjo kwenye jamii, Kuendelee kuwatumia watu maarufu kama Viongozi wa Dini, wasanii wanasiasa, wanajamii, wananzengo, wanahabari na viongozi/wazee wa kimila katika mapambano dhidi ya UVIKO – 19, Halmashauri kushirikiana na taasisi mbalimbali katika utoaji wa chanjo na hasa Taasisi kama Vyuo na Shule ili kusogeza elimu na huduma za chanjo.