Maafisa na askari 14 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA ) waliovalishwa vyeo leo Mjini Morogoro
Naibu Kamishna wa Huduma (TAWA), Prosper F. Kyssima,akizungumza katika hafla hiyo
………………………………………………….
Na.Mwandishi wetu,Morogoro
Maafisa na askari 14 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), wamevishwa vyeo vipya baada ya kupandishwa na wengine kubadilishiwa madaraja ya utumishi.
Katika hafla hiyo iliyofanyika leo, Jumamosi, Desemba 18, 2021, katika Makao Makuu ya TAWA, Morogoro,
Mgeni rasmi Naibu Kamishna wa Huduma (TAWA), Prosper F. Kyssima, akimwakilisha Kaimu Kamishna wa Uhifadhi Mabula Misungwi Nyanda, amewataka maafisa na askari hao kuvitendea haki vyeo hivyo kwa kutimiza majukumu yao kwa weledi katika maeneo yao ya kazi huku wakizingatia nidhamu ya kijeshi kwa mapana yake.
Pia amewaelekeza maafisa na askari wa TAWA kuzingatia nidhamu katika jeshi ikiwa ni pamoja na kuzingatia mahudhurio ya paredi zote
zilizowekwa kwa mujibu wa utaratibu.
Amesisitiza, wanatakiwa kumheshimu aliyewazidi na waliyemzidi cheo, kuwa nadhifu wa mavazi na mwenendo wa jumla mahali pa kazi na katika jamii.
“Ni imani yangu kwamba vyeo mlivyovishwa kijeshi vitawaongezea nidhamu, ujasiri na kujiamini pale mtakapokuwa mnatekeleza majukumu yenu,” amesema Kyssima.
Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi Operesheni, Mlage Kabange, amesema TAWA itaendelea na utekelezaji wa agizo la serikali la kubadili mfumo wa uendeshaji kutoka mtindo wa kiraia kwenda mfumo wa kijeshi, kwa maafisa na askari wake maeneo yote.
Amesema katika kuthibitisha azma hiyo, hadi sasa kuna maafisa na askari 150 wanaoendelea na mafunzo katika Chuo cha Likuyu Sekamaganga, ambao wanatarajiwa kuhitimu Desemba 22, mwaka huu.