…………………………………………………………..
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi amewataka Watendaji wa Kata na Wenyeviti wa Vijiji kutoonea wananchi wanaostahili kunufaika na Mpango wa Serikali wa kuziinua Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) huku akiwataka kutoa taarifa sahihi za watu wanaostahili kupata fedha hizo ili waweze kujikwamua kiuchumi kama lilivyo lengo la Serikali.
Ndejembi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kondo wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani ambao ni wanufaika wa mradi wa TASAF ambapo ametumia fursa hiyo kuwaonya viongozi wanaokwamisha wananchi wenye sifa kupata fedha hizo.
Amesema kama Wizara wamekua wakipokea malalamiko kwamba wapo Wenyeviti wa Vijiji ambao wamekua wakionea watu kwa kuondoa majina yao licha ya kustahili kupata fedha hizo na kuwaonya kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika.
“Rais Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake kwa watanzania alielekeza kaya zote maskini ambazo zilikua zimeachwa kwenye mpango huu tena wengine kwa uzembe wao kuandikishwa ili waweze kunufaika na fedha hizi, lengo la Rais wetu ni kuona kwamba hadi kufikia 2023 kaya zote zilizonufaika na TASAF zinanyanyuka kiuchumi.
Tunapata malalamiko kwamba viongozi wa Vijiji wanaoonea wanufaika wa TASAF, kwamba mtu anastahili kuandikishwa Mwenyekiti wa Kijiji anasema huyu anajiweza, nitoe inyo kwa viongozi wanaokwamisha wananchi kunufaika na fedha hizi tukiwabaini tutawachukulia hatua.
“Niwaagize Maafisa Kilimo, Uvuvi, Biashara na Maendeleo ya Jamii kuwatembelea wanufaika hawa wa TASAF ili kuwapa mbinu mbalimbali za nini cha kufanya wanapopata fedha hizi, ni jukumu lenu kuwasaidia ili wasitumie fedha hizi hovyo,” Amesema Naibu Waziri Ndejembi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainab Abdallah amemuahidi Naibu Waziri Ndejembi kuwa atahakikisha anasimamia utekelezaji wa maagizo yake kwa Maafisa Kilimo, Uvuvi na Biashara ili kuweza kuwasaidia wanufaika wa TASAF kutumia fedha wanazopata kuboresha maisha yao.
Naibu Waziri Ndejembi aliambatana na Naibu Katibu Mkuu Utumishi, Dk Francis, Mratibu wa TASAF Makao Makuu, Roy na watendaji wengine wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.